1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa nje wa Ujerumani na Marekani wakubaliana

Mohammed Abdulrahman
30 Agosti 2017

Ujerumani na Ulaya zinataka kuhakikisha vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Urusi havisababishi kuzuka kwa enzi mpya ya uhusiano mbaya kati ya Urusi na nchi za Magharibi

https://p.dw.com/p/2j4Ys
USA Gabriel bei Tillerson in Washington
Picha: picture-alliance/AP-Photo/S. Serkan Gurbuz

Hayo yameelezwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa  Ujerumani Sigmar Gabriel baada ya mazungumzo  na Waziri mwenzake wa Marekani Rex Tillerson mjini washington.

Waziri Gabriel alisema alizungumza na  na Tillerson jana na kuongeza kwamba  amefurahishwa  kwamba Rais Donal Trump wa Marekani amekubali kuwa na ushirikiano na washirika  wa Marekani kuhusu hatua  zaidi za baadaye. Gabriel alisema , " sisi kama Waulaya tuna wasiwasi mkubwa kwamba  hili litakuwa na athari isiyotarajiwa kwa Ulaya. Hatutaki kuharibu kabisa  uhusiano wa kibiashara na  Urusi hasa katika sekta ya nishati."

Mnamo mwezi huu Rais Trump  aliidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi kutokana na hatua yake ya kulitwaa jimbo la  ukraine la Crimea  2014, na  kwa kile kilichoelezwa na  duru za usalama  za Marekani kuwa ni kujiingiza kwa Urusi katika mchakato wa uchaguzi wa Marekani, dai ambalo Urusi imelikanusha.

Gabriel ameikosoa Marekani kwa kuchukua hatua hiyo na kwamba itasababisha makampuni ya Ujerumani yanayohusika na miradi ya nishati nchini Urusi kutozwa faini kwa kukiuka sheria ya  Marekani na kusababisha enzi ya mvutano mpya kati ya  Urusi na Marekani na pia  na nchi nyengine za magharibi.

Brigitte Zypries Bundeswirtschaftsministerin SPD
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Brigitte ZypriesPicha: picture-alliance/dpa/S. Pförtner

Kwa upande mwengine waziri wa  uchumi wa Ujerumani Brigitte Zypries ameutaka Umoja wa Ulaya  ulipize kisasi dhidi ya  Marekani ikiwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi vitapelekea makampuni ya Ujerumani kuadhibiwa.

Mwakilishi  mpya mteule wa Marekani nchini Ukraine Kurt Volker aliiambia Deutsche Welle kwamba Marekani haitokuwa na mkataba mwengine na  Urusi bila ya kuzingatia ridhaa ya ukraine au  kushauriana na  Ulaya. Alisema  Marekani imeeleza wazi inaunga mkono kikamilifu mchakato wa Normandy na haina  nia ya kuwa sehemu ya utaratibu huo au kukiuka yaliofikiwa. 

Mapema wiki hii, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa walitowa wito kuwataka wanajeshi wa Ukraine na wapiganaji wanaotaka kujitenga  wakiungwa mkono na Urusi, kuzidisha juhudi ili kuyatekeleza makubaliano ya usimamishaji mapigano.  Mzozo huo umeshasababisha kupotea kwa  maisha ya zaidi ya watu 10,000. Merkel aliwaambia  waandishi habari jana  kwamba vikwazo dhidi ya Urusi vitaondolewa pale hali  itakapoboreka, mashariki mwa Ukraine.

Gabriel leo yuko mjini Paris  alikoelekea moja kwa moja baada ya ziara yake mjini Washington.  Amekutana na  Rais Emmanuel Macron na amepangiwa pia kuhudhurai kikao cha baraza la mawaziri baada ya mazungumzo yake katika ikulu ya Elysee.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Reuters, dpa
Mhariri:Iddi Ssessanga