1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa NATO wakutana Uturuki

4 Februari 2010

Mawaziri wa Ulinzi wa nchi za Umoja wa kujihami wa NATO, kuanzia leo wanakutana huko Istanbul Uturuki, kujaribu kuchangiza upelekwaji wa wakufunzi wengi wa kijeshi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la Afghanistan.

https://p.dw.com/p/LshF
Slowakei Treffen NATO Verteidigungsminister Generalsekretär Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu waNATO Anders Fogh RasmussenPicha: AP

NATO kwa sasa ikiongoza jeshi la kimataifa la msaada wa kiusalama ISAF nchini Afghanistan, imekwishakusanya wanajeshi wa ziada wapatao 40,000 na wamekwishaanza kuwasilini nchini humo katika harakati mpya za kukabiliana na ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban.

Mawaziri hao wanakutana mnamo wakati ambapo Rais Hamid Karzai akizunguka katika nchi mbalimbali kujaribu kuunadi mpango wake mpya wa amani ya Afghanistan.

Rais huyo anatarajiwa kuwa mjini Munich katika mkutano wa kimataifa wa usalama utakaonza kesho.

Mapema wiki hii Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen alionya kuwa nchini Afghanistan kuna uhaba mkubwa wa askari polisi, na kwamba wanahitajika kiasi ya wakufunzi wa 100 kwa ajili ya jeshi la polisi.

Amesema kuwa mnamo kipindi cha miaka miwili ijayo mahitaji hayo yatakuwa makubwa zaidi, na kwamba katika mkutano huo wa leo, anawahamasisha mawaziri wa ulinzi wa NATO kuchangia wakufunzi kwa ajili ya jeshi la polisi la Afghanistan.

Jeshi la usalama la kimataifa ISAF, linatarajia kuongeza idadi ya askari polisi nchini Afghanistan kutoka 80,000 hivi sasa hadi kufikia 109,000 Oktoba mwaka huu na hadi 134,000 Oktoba mwakani.

Wakufunzi hao siyo tu kwamba wanatakiwa kwa ajili ya kazi ya kuajiri na kutoa mafunzo, lakini pia, kuboresha kiwango cha maafisa polisi waliyopo hivi sasa.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani amenukuliwa akisema kuwa kiwango cha mahitaji ya mafunzo kwa polisi wa Afghanistan ni kikubwa sana kwani ni asilimia 25 tu ya askari polisi waliyopo hivi sasa ambao wamepata mafunzo yanayotakiwa kwa kazi hiyo.

Wengi wa waliyoajiriwa hawajui kusoma, kama ilivyo kwa karibu nusu nzima ya watu wa Afghanistan, na katika wiki nane za mafunzo ya upolisi wanalazimikia kutumia mwezi mmoja darasani kujifunza kusoma, ili waweze kusoma na kuelewa leseni za madereva pamoja na makaratasi mengine muhimu.

Na wakati mawaziri hao wa ulinzi wa NATO wakianza mkutano wao huko Uturuki, nchini Afghanistan majeshi yao yanaarifiwa kujiandaa na mashambulizi makubwa kabisa dhidi ya Taliban.

Maelfu ya wanajeshi wa Afghanistan na wale wa NATO wanajiandaa kwa mashambulizi hayo huko kusini mwa Afganistan, harakati ambazo inaarifiwa kuwa huenda zikawa kubwa tokea Rais Barack Obama wa Marekani alipotangaza kuongeza idadi ya wanajeshi elfu 30 wa ziada, huku nchi nyingine wanachama wa NATO zikichangia wanajeshi elfu 10 zaidi.

Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imesema kuwa harakati hizo za kijeshi katika jimbo la Helmand zitaongozwa na jeshi la Afghanistan, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kukabidhi majukumu ya kiusalama kwa jeshi na polisi wa serikali ya Rais Karzai inayoungwa mkono na nchi za magharibi.

Msemaji wa wizara hiyo ya ulinzi ya Afghanistan, Mohamed Zahiri Azimi amesema kuwa operesheni hiyo inatayashirikisha jeshi na polisi wa Afghanistan, jeshi la Marekani pamoja na wale wa kikosi cha usalama cha kimataifa ISAF.

Hata hivyo hakuweza kuelezea tarehe haswa ambapo operesheni hiyo itaanza.

Naye msemajai wa NATO Eric Tremblay amesema kuwa watashirikiana na majeshi ya Afghanistan katika kusafisha, kudhibiti na kujenga, kwa ajili ya wananchi wote wa Afghanistan.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AFP

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman