1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika kukutana Addis Ababa

Coletta Wanjohi7 Februari 2019

Mawaziri hao kuanza mkutano wa siku mbili mjini Addis Ababa, Ethiopia, kupanga ajenda ambayo viongozi wakuu wa nchi hizo watayajadili katika mkutano wa kilele wa kila mwaka wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/3Ctey
Äthiopien Addis Abeba Afrikanische Union Gipfel Guterres
Picha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU, wanaanza mkutano wa siku mbili mjini Addis Ababa, Ethiopia, kupanga ajenda ambayo viongozi wakuu wa nchi hizo watayajadili katika mkutano wa kilele wa kila mwaka, utakaofanyika katika makao makuu ya AU tarehe 10 na 11 mwezi huu wa Februari.

Katika makao makuu ya Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia kuna mfano wa shule ambayo imeharibiwa kwa sababu ya vita. Mfano huu unaonyesha dawati zimevunjwa, mawe yametupwa ndani ya darasa , vitabu vitabu vilivyoharibiwa vikiwa vimetawanywa huku na kule.

Mfano huu umetengenezwa na kamisheni ya ajira na wafanyakazi, sayansi na teknolojia katika kamisheni ya Umoja wa Afrika. Mkuu wa kamisheni hiyo Sarah Anyang Agbor, anasema kuwa wanataka viongozi wanapokuja katika mkutano wao wa kilele kuanzia tarehe saba Februari, wakumbushwe kuwa ni lazima amani barani ipewe kipaumbele. Anyang Agbor ameendelea kusema:

" Hakuna ambaye hufikira mambo ya kuchukua vyeti vyake wakati wa maafa au vita. Kila mtu hufikiria maisha yake, kwanza , lakini unapofika unapokimbilia je utaanzaje shughuli za kujiingizia kipato? Kile ambacho hatuking'amui, ni kuwa  ikiwa hatutatatua shida zetu katika bara hilo, shida hizo tutaendelea kuishi nazo.”

Mwaka wa 2019 umechaguliwa na Umoja wa Afrika kuwa mwaka kwa ajili ya wakimbizi na waliolazimika kuyahama makaazi yao. Lengo ni kuhakikisha kuwa mwaka huu nchi za Afrika zinajitahidi kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowalazimisha watu kuyapa kisogo makaazi yao.

Takwimu zaonyesha kuwa theluthi moja ya watu milioni 68 duniani ambao wamelazimika kukimbia makwao, wapo barani Afrika.

Wengi wamehama kwa sababu tofauti mkiwemo vita, magonjwa, mabadiliko ya tabianchi na ubaguzi. Khabele Matlosa , mkurugenzi wa kamisheni ya siasa katika kamisheni ya Umoja wa Afrika anasema kuwa hili ni jambo ambalo litapewa kipaumbele katika mkutano wa umoja wa Afrika mwaka huu.

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki
Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa FakiPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

" Hapa barani tuna wakimbizi milioni sita na laki tatu na wakimbizi wa ndani ya nchi zao ni milioni 14 na nusu. Hii ni idadi kubwa. Sasa katika hali kama hii tutawezaje kama bara kutimiza matarajio yetu ya ajenda 2063 ya kibara? Tutawezaje kufikia malengo ya maendeleo ya mwaka 2030?” Amesema Matlosa

Musa Ecweru , waziri wa wakimbizi na majanga ya dharura nchini Uganda, anasema kuwa nchi yake ambayo imeshaanza kuweka sera za kuwapa wakimbizi haki za kuishi kama wakaazi wa nchi, ipo tayari kutoa mfano wake kwa nchi zingine katika mkutano wa mwaka huu. Ecweru ameongeza kuwa:

" Tunachojua na kuamini kama Uganda ni kuwa tukiwatayarisha wakimbizi kuwa na ujuzi wakiwa nchini kwetu , watakaporejea nyumbani kwao wataweza kwenda kujenga tena nchi zao. Hii ni tofauti na ikiwa tungewaacha wabaki vile tu walivyokuja bila ujuzi wowote.”

Mkutano wa marais pia utajadili vita na mizozo inayoendelea katika Ukanda wa SAHEL, bonde la  ziwa Chad, na katika jamhuri ya Afrika ya Kati . Khabele Matlosa , mkurugenzi katika kamisheni ya maswala ya siasa katika kamisheni ya Umoja wa Afrika anasema kuwa vitisho vya usalama vitajadiliwa na viongozi.

" Ukanda wa Kusini mwa Afrika hadi hivi majuzi ulidhaniwa kuwa sehemu ya usalama bila shida za ugaidi wa vita, lakini sasa hivi majuzi tumeona ugaidi ukiibuka Msumbiji, haya ni maswala yanasababisha hofu katika Umoja wa Afrika, ya yatajadiliwa.

Rais Paul Kagame wa Rwanda atawaarifu viongozi wenzake kuhusu maendeleo katika utekelezaji wa mpango wa mabadiliko katika oparesheni ya muungano wao na kamisheni ya Umoja wa Afrika, kama marais walivyopendekeza afuatilie.

Mkutano wa viongoizi wa Afrika pia utajadili swala la utekelezwaji wa eneo huru la biashara, mradi ambao unanuiwa kusaidia nchi za Afrika kujitegemea kiuchumi kwa kufanya biashara baina yao.

Umoja wa Afrika unasema kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo , Felix TShisekedi anatarajiwa kuhudhuria mkutano huu wa umoja wa Afrika.

Mwandishi: Coletta Wanjohi/DW-Addis Ababa

Mhariri: Daniel Gakuba