1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa kigeni Ulaya kujadili msaada zaidi kwa Ukraine

23 Januari 2023

Hakuna maamuzi rasmi yatayotarajiwa Brussels kuhusu msaada kwa Ukraine ingawa kuhusu Iran Umoja wa Ulaya unatarajiwa kutangaza majina 37 ya Wairan watakaowekewa vikwazo

https://p.dw.com/p/4MZpq
Luxemburg | Treffen der EU-Außenminister
Picha: Virginia May/AP Photo/picture alliance

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana Brussels kujadili suala la kuipatia msaada wa ziada Ukraine, lakini pia wanatarajiwa kujadili kuhusu Iran na kutangaza majina zaidi kwenye orodha ya wairan waliowekewa vikwazo kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo wa Ulaya Josep Borrell akiwasili kwenye mkutano wa Brussels wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja huo amesema anataraji nchi 27 wanachama zitaidhinisha fungu jingine la euro milioni 500 za msaada wa kijeshi kwa ajili ya Ukraine.

Luxemburg | Treffen EU-Außenministertreffen | Josep Borrell
Picha: Lenoir/EUC/ROPI/picture alliance

Fedha hizo kwa mujibu wa Borrell ni sehemu ya kile kinachoitwa hazina ya amani ya Umoja wa Ulaya ambayo ni bajeti ya ziada ya kuuwezesha Umoja huo kuwa tayari  kusimamia usalama duniani.

Wiki iliyopita zilikuwepo ripoti zilizoonesha kwamba Hungary iliipinga hatua hiyo ingawa hii leo waziri wa mambo ya nje na msemaji wa serikali ya mjini Budapest alikataa kutoa tamko lolote kuhusu ripoti hizo.

Upande mwingine kuhusu suala la vifaru vya kivita,waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baebock amesema Ujerumani haiwezi kuizuia Poland ikiwa nchi hiyo inataka kupeleka vifaru vya kivita chapa Leopard nambari 2 nchini Ukraine.

Waziri mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki amesema nchi yake itaiomba ridhaa Ujerumani kuhusu kupeleka vifaru hivyo vya kivita.Mtazamo uliotolewa na  Ujerumani unaonesha kuna uwezekano wa kupatikana mwafaka juu ya suala hilo. Nchi za Umoja wa Ulaya pia zinashughulikia suala la vikwazo kadhaa vinavyotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao dhidi ya Urusi kufuatia uvamizi wake wa kijeshi nchini Ukraine.

Deutschland Bundeswehr Kampfpanzer Leopard 2 A7V
Picha: Philipp Schulze/dpa/picture-alliance

Hayo yameelezwa na vyanzo vya kidiplomasia ingawa vilevile imetajwa kwamba hakuna maamuzi yanayotarajiwa kutolewa kwenye mkutano wa leo.

Kadhalika mawaziri wa mambo ya nje watajadili kuhusu kutumia mali ya Urusi iliyozuiwa katika nchi za Umoja huo ambazo ziko chini ya vikwazo zikijumuisha akiba ya fedha euro bilioni 300 ambazo zitatumiwa kusaidia kuijenga upya Ukraine.Zelensky ayapongeza majeshi yake kuyakomboa maeneo ya kusini

Ama kuhusu Iran mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema hawawezi kuliorodhesha jeshi la ulinzi wa mapinduzi ya Iran katika orodha ya magaidi hadi pale mahakama ya Umoja huo wa Ulaya itakapotowa uamuzi wa kusema ni magaidi.

Hata hivyo mawaziri wanaokutana Brussels wameshajiandaa kuyaongeza majina 37 ya Wairan na taasisi za nchi hiyo katika orodha ya Umoja wa Ulaya ya vikwazo kufuatia ukikwaji wa haki za binadamu unaofanyika katika Jamhuri hiyo ya kiislamu.

Brüssel EPRS Policy Roundtable | Zehn Themen in 2023 | Herausforderungen und Entscheidungen in Zeiten von Krisen und Krieg
Picha: Philippe Buissin/EP

Bunge la Umoja huo wiki iliyopita lilitowa mwito wa jeshi la kimapinduzi la Iran litiwe kwenye orodha ya magaidi kufuatia ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wa Iran pamoja na hatua yake ya kuipelekea Urusi droni.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW