1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha wa G7 wanakutana Italia

Sylvia Mwehozi
12 Mei 2017

Mawaziri wa fedha wa nchi saba zilizoendelea kiuchumi na kiviwanda duniani G7 wanakutana Ijumaa(12.05.2017) katika mji wa Bari, Italia kutafuta misingi ya pamoja na utengamano juu ya mustakabali wa baadaye wa biashara.

https://p.dw.com/p/2cquc
G7 Finanzgipfel
Picha: picture alliance/AP Photo/C.Fusco

Mkutano huo utakaoendelea hadi Jumamosi(13.05.2017), ni wa kwanza kwa kundi la nchi za G7 kuhudhuriwa na waziri wa fedha wa utawala wa Trump, Steven Mnuchin, ambaye anatazamiwa kuwasilisha ajenda ya kiuchumi ya Marekani.

Lakini kwa ujumla maafisa kutoka nchi zote saba zilizo tajiri na mageuzi makubwa ya kiviwanda wameashiria kwamba utofauti juu ya mipango ya Rais Trump ya kuweka mipaka ya biashara imewekwa kando.

Mwenyeji Italia amefikiria kutafuta maeneo ambako wanaweza kufikia makubaliano baina ya Trump lakini bado ajenda hazieleweki na vipaumbele vya mshirika mkuu Washington kwa nchi za Ulaya, Canada na Japan. Waziri wa fedha wa Italia, Pier Carlo Padoan, wakati akiwasili amegusia yatakayotawala mkutano huo, "tunazo mada nyingi, hata kodi na ningependa kupata usikivu wenu juu ya ukuaji na ushiriki wa kijamii ambao umekuwa ni mada muhimu kwa G7 pamoja na G20. Nina furaha kwamba Italia inatekeleza haya. Ipo misamamo tofauti ya mataifa lakini G7 ni muhimu na tunazungumza katika mtazamo wa kawaida na kuufanyia kazi."

Pier Carlo Padoan
Waziri wa fedha wa Italia Pier Carlo Padoan Picha: OECD / nc / nd

Biashara ni ajenda itakayotawala mazungumzo ya pande mbili baina ya Japan na Ujerumani , kwa kuwa nchi hizi mbili ni wauzaji wakubwa na wanatuhumiwa na Trump kwamba wamekuwa wakifaidika isivyo sawa kutokana na viwango vya kubadilisha Dola.

Masuala mengine yaliyoko mezani mwa mkutano huo ni pamoja na ukwepaji kodi kimataifa ikiwemo udhibiti wa mitandao kimataifa, kupambana na ufadhili wa ugaidi, utetezi wa taasisi za fedha dhidi ya mashambulizi ya kimtandao na namna gani ya kuhakikisha faida za ukuaji zinagawiwa sawasawa.

La mwisho ni suala ambalo limekuwa katika ajenda za G7 tangu mgogoro wa kifedha wa 2007-2008. Lakini limepewa nyongeza ya udharura baada ya kura ya Uingereza ya kujiondoa Umoja wa Ulaya na ushindi wa Trump, majanga ambayo yanahusishwa na madhara hasi ya mwenendo wa kiuchumi wa hivi karibuni kwa idadi ya watu.

Treffen der G7-Finanzminister und -Notenbankchefs
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble katika mkutano wa G7Picha: picture alliance/dpa/A.Medichini

Kauli za Trump wakati na baada ya kampeni za uchaguzi zinaashiria kuwa ni mtu anayependelea "ukuaji shirikishi" na waziri wake Mnuchin ameelezea wajibu wake muhimu kuwa ni kuongeza kipato kwa wafanyakazi wa Marekani.

Mkutano huu ni wa kwanza tangu kiongozi wa sera za mrengo wa kati Emanuel Macron alivyochaguliwa kuwa rais, ingawa nchi yake itawakilishwa na waziri wa kisosholisti anayemaliza muda wake Michel Sapin.

Macron ni mfanyabiashara huru lakini pia ni muungaji mkono mkubwa wa Muungano wa Ulaya na anaamini Umoja huo unapaswa kutumia misuli yake ya kimataifa kuhakikisha milango ya masoko haipelekei bidhaa zake kuathiriwa na zile za nje.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef