1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha wa G7 wakutana Ufaransa

17 Julai 2019

Mawaziri wa fedha kutoka kundi la mataifa saba tajiri zaidi duniani wameanza mazungumzo mjini Chantilly kaskazini mwa Paris yanayolenga kusaka msimamo wa pamoja wa suala tata la kodi kwa makampuni makubwa ya teknolojia

https://p.dw.com/p/3MCxc
Frankreich St. Malo Flaggen
Picha: DW/Bernd Riegert

Mwenyeji wa mkutano huo, waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire anaungana na wenzake hii leo kwenye mkutano huo unaoyakutanisha mataifa hayo ambayo ni Ujerumani, Uingereza, Italia, Canada, Japan na Marekani.

Mawaziri hawa wanakutana katika wakati ambapo kuna sintofahamu kuhusiana na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia pamoja na sera za biashara za rais wa Marekani Donald Trump za Marekani Kwanza, zilizosababisha vita vya kibiashara na China, na hali ya wasiwasi na Ulaya.

Mkutano huu unaandaa mpango mkakati wa mkutano wa kilele utakaowakutanisha wakuu wa serikali na mataifa yaliyostawi kiviwanda ya G7, unaotarajiwa kufanyika kati ya Agosti 24 na 26 katika mji wa Basques, nchini Ufaransa.

Mawaziri hawa pia wanatofautiana kuhusu namna bora zaidi ya kuyakata kodi makampuni makubwa ya teknolojia. Ufaransa inataka kuutumia vizuri uenyekiti wa mkutano huu wa siku mbili kupata uungaji mkono mpana katika kuhakikisha kunakuwepo na kiwango cha chini cha makato hayo ya kodi kwa mashirika.

Bruno Le Marie | französischer Finanzminister
Bruno Le Maire, waziri wa fedha wa Ufaransa anataka kutumia nafasi hiyo kushawishi uungaji mkono wa suala hilo la kodiPicha: imago/panoramic/G. Roussel

Serikali za G7 zina wasiwasi kwamba sheria za kimataifa za kodi za miongo mingi zinakabiliwa na msukumo mkubwa kutokana na kuibuka kwa makampuni ya Facebook na Appleambayo yanajipatia faida kubwa na hususan kutoka mataifa yanayotoza kiwango cha chini cha kodi, bila ya kujali chanzo cha msingi cha mapato hayo.

Suala hili limeibua ghadhabu katika siku za hivi karibuni, wakati Ufaransa ilipompuuza waziwazi rais Donald Trump wiki iliyopita na kupitisha kodi kwenye mapato ya makampuni makubwa ya kidijitali nchini Ufaransa, licha ya kitisho kutoka kwake  cha kuanzisha uchunguzi unaoweza kusababisha kuwekewa ushuru wa bidhaa.

Waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire alisema jana kwamba Ufaransa ni taifa huru na litaendelea kufanya maamuzi kama taifa huru kuhusu masuala yote yahusuyo kodi, "Ninataka kusema kwamba zipo namna nyingine za kusuluhisha tofauti kati ya washirika kuliko vitisho. Ninataka kusema pia kwamba Ufaransa ni taifa huru linalofanya maamizui kwa njia huru katika sera zake za kodi na kwa hiyo litaendelea kuamua kuhusu sera zake za kifedha kwa namna huru."

Lakini tofauti na mvutano baina yao, Marekani na Ufaransa wanaunga mkono kanuni za kuhakikisha kunakuwepo na kiwango cha chini cha kodi kama sehemu ya juhudi za miongoni mwa mataifa 139 za kufanyia mrekebisho makubwa kanuni hizo za kimataifa za kodi.

Ingawa makubaliano ya G7 yataweza kufungua njia ya kupatikana kwa msukumo mpana zaidi, lakini makubaliano baina ya mawaziri wote wa mataifa hayo kuhusu kiwango cha chini ama tofauti ya viwango huenda yakawa magumu kufikiwa kwa sababu Uingereza na Canada zina wasiwasi kuhusu viwango hivyo.