1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha wa G7 kujadili uchumi wa dunia Dresden

27 Mei 2015

Mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu kutoka mataifa ya kundi la G7 wanakutana mjini Dresden mashariki mwa Ujerumani, kujadili mwelekeo wa chumi kubwa za dunia na pia mgogoro unaoitishia Ugiriki.

https://p.dw.com/p/1FX24
G7 England Gruppenbild
Picha: Getty Images

Baada ya kuanza mwaka huu kwa mafanikio, ukuaji wa uchumi wa dunia unaonekana kusimama, ukiongozwa na kupungua kwa kasi nchini Marekani, China na Ujerumani. Ukuaji nchini Japan pia haujafikia matarajio.

Kwa mara ya kwanza katika miaka kadhaa, kanda inayotumia sarafu ya euro imejitokeza kama eneo la kutia matumaini, wakati ambapo ishara zinaonyesha mageuzi magumu ya kiuchumi yanaanza kuzaa matunda katika mataifa kama vile Uhispania na Ireland, ambayo yalikuwa kitovu cha mgogoro wa muda mrefu wa madeni katika kanda hiyo.

Lakini kinachojitokeza zaidi katika kanda hiyo yenye wanachama 19 ni mkwamo mzito kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake, huku kukiwa na wasiwasi kwamba huenda nchi hiyo hatimaye ikaachana na matumizi ya sarafu ya euro.

Viongozi wakuu wa mataifa yanayounda kundi la G7.
Viongozi wakuu wa mataifa yanayounda kundi la G7.Picha: Reuters

Mkutano wa Dresden, ambao utamalizika siku ya Ijumaa, unafanyika pia huku zikiwa zimetolewa data mpya za ukuaji wa kiuchumi duniani, zikiwemo takwimu ambazo wachambuzi wengi wanatabiri zitaonesha kuwa uchumi wa Marekani ulisinyaa katika robo ya kwanza ya mwaka.

Mashaka katika masoko ya fedha

Hili matokeo yake huenda likazidisha mashaka yaliyotanda katika masoko ya fedha kuhusiana na muda unaosubiriwa sana, wa upandishaji wa viwango vya riba na benki kuu ya Marekani, ambao utakuwa wa kwanza tangu kuanza kwa mgogoro wa kifedha miaka saba iliyopita. Kikao cha kesho Alhamisi kuhusu matarajio ya uchumi wa dunia, kitahusisha mkutano rasmi kati ya mawaziri na magavana wa benki kuu za mataifa yao.

Ukiongozwa na waziri Wolfgang Schäuble wa Ujerumani, mkutano wa mawaziri wa fedha utahudhuriwa na Joe Oliver wa Canada, Michel Sapin wa Ufaransa, Carlo Padoan wa Italia, Taro Aso wa Japan, George Osborne wa Uingereza, na Jacob Lew wa Marekani. Ujerumani kwa sasa ndiyo inashikilia urais wa kundi la G7.

Mkutano wa Dresden utasaidia pia kuandaa mazingira ya mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa ya G7 mwezi ujao, ambao utaongozwa na Kansela Angela Merkel na utafanyika katika jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani.

Mawaziri hao wa fedha wanatarajiwa kuidhinisha hatua kadhaa kama vile kuimarisha vita dhidi ya ufadhili wa ugaidi, kupunguza mzigo wa madeni wa Ugiriki, kukandamiza ukwepaji kodi na kutoa wito wa juhudi zaidi katika mageuzi ya kimuundo.

Lakini masuala yenye utata zaidi yanaweza yasiwepo kwenye ajenda ya Dresden, lakini yatagubika mijadala kandoni mwa mkutano huo. Hayo yanatarajiwa kuhusisha mgogoro wa madeni wa Ugiriki, na pia hatari ya kura ya maoni inayopangwa na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kuhusu kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Nembo ya Mkutano wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu za mataifa ya G7.
Nembo ya Mkutano wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu za mataifa ya G7.

Wanne kati ya wadau muhimu katika mgogoro wa Ugiriki - Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF Christine Lagarde, rais wa Benki kuu ya Ulaya ECB Mario Draghi, mwenyekiti wa kundi la mawaziri wa fedha wa kanda ya euro Joroen Dijsselbloem na Kamishna wa uchumi na fedha wa Umoja wa Ulaya Pierre Moscovici watahudhuria mkutano wa Dresden.

Ujerumani kuwekewa mbinyo

Marekani huenda ikautumia mkutano huo kuhuisha shinikizo kwa Ujerumani kuchukuwa hatua ili kusaidia kuchochea uchumi wa dunia kwa kuzindua programu mpya za uwekezaji wa umma kwa lengo la kuboresha mahitaji ya ndani.

Zaidi ya hayo, Berlin huenda pia ikabinywa kutokana na msimamo wake mkali kuhusu kukaza mkwiji, ikiwemo kutoka washirika wake kadhaa wa kanda ya euro kama vile Italia. Tayari waziri Schäuble alionya wiki iliyopita dhidi ya ufadhili wa miradi hiyo kupitia program za ukopaji wa serikali.

Wakati kukiwa na uwezekano mdogo wa kuafikiana kuhusu hatua za kuchochea mzunguko wa fedha kwenye mkutano huo, mkutano huo angalau utasisitiza umuhimu wa benki kuu za mataifa makubwa katika kuongoza ukuaji wa kiuchumi, kwa kundelea kuregeza sera ya fedha.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae

Mhariri: Daniel Gakuba