1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha wa G-7 wakutana Ujerumani

P.Martin9 Februari 2007

Mawaziri wa fedha na marais wa benki zinazotoa noti wa nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda G-7 wanakutana Essen nchini Ujerumani mwishoni mwa juma.

https://p.dw.com/p/CHKS

Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni udhaifu wa sarafu ya Japan-Yen kulinganishwa na Euro na Dola,mageuzi katika Fuko la Fedha la Kimataifa-IMF na uwekezaji imara barani Afrika.

Mkutano wa nchi 7 muhimu,zilizoendelea kiviwanda, yaani Ujerumani,Marekani,Uingereza,Japan,Kanada, Ufaransa na Italia,utahudhuriwa pia na mawaziri wa fedha wa Urussi,China,India,Afrika ya Kusini, Brazil na Mexiko walioalikwa.Kipaumbele cha waziri wa fedha wa Ujerumani,Peer Steinbrück kama mwenyeji wa mkutano huo,ni zile hatari zinazotokana na dhamana.Tangu muda mrefu,serikali ya Ujerumani imehimiza uwepo uwazi katika soko la dhamana,kwani katika juhudi ya kuzipatia sarafu za ulimwengu faida kubwa,hisa na masoko ya malighafi hubahatisha na hujitumbukiza hatarani. Baadhi kubwa ya mashirika hayo yana makao yake nchini Marekani au Uingereza.Pesa zinazotumiwa kubahatisha ni za wawekezaji wa binafsi au taasisi mbali mbali.

Kila mwaka dhamana za aina hiyo,huwapatia wawekezaji faida ya asilimia 30 au hata zaidi, jambo ambalo huzidi kuwavutia watu.Lakini dhamana hizo zinazobahatishwa zikienda kombo,maafa yake ni makubwa na muundo wa benki duniani huathirika na huweza kusababisha mzozo wa kifedha kote duniani.

Katibu katika wizara ya fedha ya Ujerumani,Thomas Mirow alisema kuwa hiyo ni mada inayoweza kujadiliwa kimataifa tu na hilo hudhihirisha umuhimu wa mkutano wa G-7. Mashirika mengi ya dhamana hufanya kazi sehemu mbali mbali za dunia na hayana makao barani Ulaya.Mada ya uwazi haina maana,pasipokuwepo ushirikiano wa Marekani.

Hata udhaifu wa sarafu ya Yen utajadiliwa na mawaziri wa fedha wa Ulaya pamoja wenzao kutoka Japan.Kwani tangu mwanzo wa mwaka jana,sarafu ya Yen kulinganishwa na Euro,imepoteza thamani yake kwa asilimia 11.Na kulinganishwa na Dola,thamani yake imeshuka kwa asilimia 4.Matokeo ni kuwa mauzo ya nje ya Japani yameimarika wakati ambapo ni vigumu kwa nchi za Ulaya na hasa Marekani kuuza bidhaa zao nchini Japan.

Kwa upande mwingine,wanaharakati wanaopinga utandawazi wanajitayarisha vile vile kufanya maandamano hiyo kesho,kati-kati ya mji wa Essen. Polisi wanataraji kuwa kati ya watu 500 hadi 2,000 watashiriki katika maandamano hayo na yatakwenda kwa usalama.