Mawaziri wa Afrika kaskazini waafikiana kupambana na Al Qaeda.
17 Machi 2010Mawaziri kutoka mataifa hayo saba ya Burkina Faso, Chad, Libya, Mali, Mauritania, Niger na wenyeji, Algeria, ambayo yako katika jangwa la Sahara wamekamilisha mazungumzo yao kwa kuelezea azma yao ya kukomesha ugaidi katika eneo hilo.
Waziri wa Algeria anayeshughulikia masuala ya Afrika Kaskazini na Afrika, Abdelkadir Messahel, anasema: kwa msimamo uliowazi wamelaani tabia ya ulipaji fidia na watu kutekwa nyara, na kusisitizia wajibu wa kila nchi kulitekeleza kikamilifu azimio la Umoja wa Mataifa juu ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya mkutano huo wa faragha wa siku moja, alisema wamefikia muwafaka kamili katika kupambana na ugaidi katika eneo hilo, na kwamba mikakati ya utendaji huo itakuwa ni uamuzi wao. Alieleza kwamba mkakati wao wa utendaji ni uamuzi wao wenyewe, na watafanya mkutano kati ya maafisa wa jeshi na wataalamu wa kupambana na ugaidi katika eneo hilo, mkutano ambao utafanyika mwezi April katika mji mkuu wa Algeria, Algiers.
Mkutano huo ambao utakuwa wa ngazi ya wakuu wa majeshi, utajadili juu ya kuanza kushirikiana katika kufanya kazi pamoja katika kupambana na vitisho hivyo vya Al Qaeda katika eneo hilo.
Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Algeria, Mourad Medelci, alisema hayo awali baada ya kutoa wito wa kuweko ushirikiano mzuri katika mipaka ya nchi hizo. Alilaani kuzidi kuweko mafungamano kati ya ugaidi na makundi ya uhalifu katika eneo hilo ambako biashara ya magendo ya madawa ya kulevya na silaha imeongezeka.
Matawi ya Al Qaeda katika Afrika Kaskazini pamoja na makundi mengine ya uhalifu yamekuwa yakilitumia eneo kubwa la Sahara na Sahel kujificha ili wasikamatwe baada ya kufanya mashambulio ama kuteka nyara raia wa kigeni.
Al Qaeda katika eneo la Afrika Kaskazini Maghreb, ambalo linaendesha shughuli zake kutokea Algeria, limefanya mashambulio kadhaa nchini humo katika kipindi cha mwaka 2007, likiwemo shambulio la kujitolea mhanga lililolenga msafara wa rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika, ambalo liliuwa watu 22 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 100.
Vitisho vya Al Qaeda katika eneo hilo la Sahel vilichukuliwa kwa uzito wa juu baada ya kifo cha mtalii wa kiingereza, Edwin Dyer, katikati ya mwaka uliopita, ambapo kundi hilo la Al Qaeda lilimuua baada ya Uingereza kukataa kutekeleza vitisho vilivyotaka itolewe fidia, miezi sita baada ya kumkamata .
Wakati huohuo, Marekani imezikaribisha juhudi hizo za mataifa ya Afrika Kaskazini za kuimarisha ushirikiano wake katika kupambana na ugaidi.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp, Reuters)
Mhariri: Miraji Othman