1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawakili wa Mbowe waitaka mahakama kumuachilia huru

Hawa Bihoga31 Agosti 2021

Jopo la mawakili wa Freeman Mbowe imeiomba mahakama kumuachilia huru mteja wao wakidai mahakama hiyo haina mamalaka kisheria kusikiza kesi hiyo.

https://p.dw.com/p/3zjhx
Tansania | Prozess gegen Chadema Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/DW

Kesi nambari kumi na sita ya makosa ya uhujumu uchumi ndani yake kukiwa na makosa ya ugaidi, inasikizwa kwa mara ya kwanza katika mahakama kuu divisheni ya uhujumu uchumi ambapo upande wa utetezi umesema mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo inayomkabili mbowe na wenzake watatu.

Jopo la mawakili wa mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, wakiendelea kutetea hoja yao wameiambia mahakama kuwa, kwa mujibu wa sheria ya kuzuia ugaidi kesi yao inapaswa kuskizwa na mahakama kuu ya kawaida na si hiyo ambayo ni divisheni maalum kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi. Wakili wa utetezi Peter Kibatala amewaambia wanahabari.

''Tumesema kwamba mahakama hii haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo, kwa maana kwamba ni kesi ya ugaidi na tumeiomba mahakama ikikubaliana na hoja zetu basi iwaachie huru washitakiwa.'', alisema Kibatala.

Upande wa serikali ukiongozwa na wakili Robart Kidando wameiambia mahakama kwamba, kupitia marekebisho ya sheria nambari tatu ya sheria mbalimbali ya mwaka 2016 ilifanya makosa chini ya sheria ya ugaidi kuwa makosa ya uhujumu uchumi, hivyo mahakama hiyo ya rushwa na uhujumu uchumi ni sahihi kwa kesi hiyo inayomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Wito wa maridhiano ya kitaifa

Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaendelea kushikiliwa mjini Dar es Salam
Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaendelea kushikiliwa mjini Dar es SalamPicha: Ericky Boniphace/DW

Jaji Elinazer Luvanda ambae amesikiliza shauri hilo kukiwa na ulinzi mkali katika mahakama hiyo askari polisi waliojihami kwa silaha za kutuliza ghasia, mbwa na hata farasi ameahirisha shauri hilo hadi hapo kesi atakapotolea uamuzi endapo mahakama inayo mamlaka ya kusikiliza shauri hilo au kumuachilia Freeman Mbowe na wenzake.

Peter kibatala anayeongoza jopo la mawakili wa Mbowe amewaambia waandishi habari kuwa endapo hoja zao zitakataliwa, wataendelea kuwapigania wateja wao kutumia vifungu vya sheria.

Shauri hilo lililosikilizwa kwa zaidi ya saa tatu limehudhuriwa na viongozi wengine wa vyama vya upinzani na wawakilishi wa baadhi ya balozi ikiwemo Uingereza na Marekani, asasi za kiraia na viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho.

James Mbatia mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi ameiambia DW kuwa kesi hiyo inaathiri vyama vya upinzani kwani muda mwingi wanatumia kuwasili mahakamani ili kujua mwendo wa kesi hiyo, hivyo anatoa wito wa maridhiano ya kitaifa.