Mauzo ya silaha yaongezeka Mashariki ya Kati
12 Machi 2018Kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya Stockholm inayohusika na masuala ya amani ya SIPRI- mauzo ya silaha katika mataifa ya Mashariki ya Kati yaliongezeka kwa asilimia 103 katika kipindi cha mwaka 2013-2017 kulinganisha na miaka mitano iliyotangulia.
Mtafiti wa taasisi ya SIPRI, Pieter Wezeman katika taarifa yake anasema kuongezeka kwa migogoro katika mashariki ya Kati na wasiwasi kuhusu haki za binadamu kumepelekea kuwepo mijadala ya kisiasa ulaya magharibi na Amerika ya Kaskazni juu ya haja ya kuzuia mauzo ya silaha.
Hata hivyo Marekani na nchi za ulaya zinasalia kuwa wauzaji wakuu wa silaha na zilisafirisha zaidi ya asilimia 98 ya silaha zilizoingizwa nchini Saudi Arabia anasema mtafiti huyo.
Saudi Arabia inayoongoza kampeni kubwa ya kijeshi dhidi ya waasi wahouthi nchini Yemen imeshuhudia ununuzi wake wa silaha ukiongezeka kwa asilimia 225 katika kipindi cha kati ya mwaka 2013-2017 kulinganisha na mwaka 2008 hadi 2012.
Saudi Arabia ambayo ni nchi ya pili duniani kuagiza silaha kwa wingi ikitanguliwa na India wiki iliyopita ilikubali kununua ndege 48 za kisasa za kivita kutoka shirika la BAE Systems la Uingereza mnamo wakati wanaharakati wa haki za binadamu wakiikisoa Saudi Arabia kuwa inatumia silaha hizo zilizonunuliwa kutoka nchi za magharibi kuwaua raia wasio na hatia nchini Yemen.
Marekani yaongoza kwa kuuza silaha nyingi
Utafiti huo wa SIPRI umezidi kubainisha kuwa Marekani ilidhihirisha kuwa ndio nchi inayoongoza duniani kwa kuuza silaha nyingi zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ikiuza karibu theluthi moja ya silaha huku mauzo ya silaha katika mataifa ya Mashariki ya Kati yakiwa ni nusu ya silaha zilizouzwa kutoka Marekani katika kipindi hicho.
Kulingana na mikataba iliyosainiwa wakati wa utawala wa rais Barack Obama , mauzo ya Marekani ya silaha katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013- hadi 2017 yalifikia kiwango cha juu kabisa kulinganisha na mauzo ya nchi hiyo yaliyofanyika hadi mwishoni mwa miaka ya 1990.
Mikataba hii pamoja na mikataba mingine mikubwa iliyosainiwa mwaka 2017 inaashiria Marekani itaendelea kusalia kuwa nchi inayouza silaha kwa wingi zaidi katika miaka ijayo.
Urusi, Ufaransa, Ujerumani na China zimeungana na Marekani na kuwa nchi kubwa zinazo ongoza kwa mauzo ya silaha.
Mauzo ya silaha kutoka Ujerumani ambayo inashika nafasi ya nne kwa mauzo ya nje ya silaha yalishuka kwa asilimia 14 kati ya mwaka 2008 hadi 2012 na katika kipindi cha kati ya mwaka 2013 hadi 2017.
Hata hivyo mauzo ya silaha kutoka Ujerumani kwa nchi za Mashariki ya Kati yalipanda kwa asilimia 109 huku Ujerumani mwaka huu ikisema itazuia kuidhinisha mauzo hayo kwa yeyote anayejihusisha katika mgogoro nchini Yemen.
Mwandishi:Ashutosh Pandey
Tafsiri : Isaac Gamba/dw
Mhariri : Gakuba. Daniel