Mauaji yaongezeka kwa asilimia 7 Afrika Kusini
11 Septemba 2018Kiwango cha mauaji nchini Afrika Kusini ambacho tayari ni kikubwa mno kimeongezeka kwa asilimia saba, na kumlazimu waziri anayehusika na jeshi la polisi kuilinganisha hali hiyo na "uwanja wa kivita."
Polisi ilitoa takwimu za uhalifu siku ya Jumanne zikionyesha watu 20,336 waliuawa nchini Afrika Kusini kati ya Aprili 2017 na Machi, ikilinganishwa na watu 19,016 waliouawa katika mwaka uliotangulia.
Waziri wa polisi Bheki Cele, anasema kiwango hicho cha juu cha mauaji "kinakaribiana na uwanja wa kivita - wakati kuna amani na hakuna vita."
Matukio mengi ya mauaji yamehusishwa na vurugu za magenge ya uhalifu katika mkoa wa Cape Magharibi, ambao mji wake mkuu ni Cape Town.
Kamati ya bunge inasema juhudi za polisi kukabiliana na tatizo hilo hazijakuwa na ufanisi na kwamba makamanda wanapaswa kuimarisha uwepo wa usimamizi wa sheria katika maeneo yenye matukio mengi ya uhalifu.
"Kamwe isitokee tena tukaja hapa kutoa takwimu kama hizo. Haiwezekani kwamba Waafrika Kusini wanaishi katika hofu kama hiyo, msongo kama huo na mauaji kama hayo," alisema Cele.
Matukio ya mauaji yaliongezeka kwa asilimia 6.9 katika mwaka wa kifedha wa 2017-18, ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia, kwa mujibu wa takwimu hizo. Mauaji ya wanawake na watoto yaliongezeka pia.
Ubakaji uliongezeka kwa asilimia 0.5, ambapo matukio 40.035 yalirekodiwa ikilinganishwa na matukio 39,828 ya mwaka uliotangulia, kwa mujibu wa takwimu hizo za polisi.
Afrika Kusini inajulikana kimataifa kutokana na uhalifu wake wa vurugu, lakini takwimu za kila mwaka zinapingwa mara kwa mara, hususani tarakimu kuhusu ubakaji.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, ape
Mhariri: Lillian Mtono