Mauaji yaendelea Syria, wapiganaji wa kigeni wahusishwa
27 Novemba 2012Kulingana na Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London, gari lililokuwa lililotengwa mabomu liliripuka karibu na kizuizi kimoja cha polisi katika eneo la Jdeidet Artuz na kusababisha vifo vya wanajeshi wawili.
Mapigano yamepamba moto karibu na mji mkuu Damascus baada ya jeshi la serikali kuanzisha operesheni ya kuwaondoa waasi katika maeneo wanayoyashikilia. Waasi wameweka kambi zao maalum mjini Damascus ambako vikosi vya serikali vinataka kuingia.
Mapigano yasambaa
Mapigano mengine pia yaliripotiwa katika maeneo ya Moadamiyet al-Sham karibu na mji wa Daraya, ambapo mwezi wa Agosti kulifanyika mauaji ya halaiki na watu takriban 500 kuuawa. Mjini Idlib nako kaskazini magharibi mwa Syria kumekuwa na mashambulizi ya anga na watu watano wanaripotiwa kuuwawa huku wengine 30 wakijeruhiwa.
Mkurugenzi wa Shirika hilo la Haki za Binaadamu, Rami Abdel Rahman, akizungumza na shirika la habari la AFP amesema kuwa wamefanikiwa kuandika majina ya wale wote waliojeruhiwa na pia kuuwawa katika mashambulizi ya angani yaliyotokea kilomita mbili magharibi mwa mji mkuu Damascus.
Tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano nchini Syria kuupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad Machi 2011, takriban watu 40,000 wameshauawa huku wengine wengi wakipoteza makaazi yao.
Wapiganaji wa kigeni
Huku hayo yakiarifiwa hii leo gazeti moja la Syria limechapisha majina ya wapiganaji wa kigeni 142 kutoka nchi 18 wanaosemekana kuuwawa pamoja na waasi katika mgogoro huu wa Syria. Gazeti hilo la Al-Watan linalounga mkono utawala wa Syria limesema tayari serikali ya Syria imeiwasilisha orodha hiyo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita.
Gazeti imesema wapiganaji hao iliowaita magaidi wanaohusishwa na al-Qaida, ni kutoka nchi za Kiarabu, kaskazini mwa Afrika na Ghuba na kwamba kati yao kuna raia wa Saudi Arabia, Misri, Qatar, Azerbaijan, Chad, Chechnya, Afghanistan na Uturuki.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman