Huko kaskazini mwa Afghanistan, wanachama kumi wa kikundi cha
kimataifa cha madaktari, akiwemo Mjerumani, wameuliwa kwa risasi.
Jambo hilo limearifiwa na msemaji wa Jumuiya ya Kikristo yenye
kutoa misaada, International Assistance Mission, mjini Kabul, Licha
ya Mjerumani, miongoni mwa waliouliwa kuna Muingereza,
Wamarekani sita, akiwemo mwanamke, na Wa-Afghani wawili
waliokuwa wakalimani. Mwanachama mmoja wa Ki-Afghani katika
kundi hilo aliiarifu jumuiya hiyo juu ya shambulio hilo. Wataliban
wenye itikadi kali za Kiislamu wamechukuwa dhamana ya shambulio
hilo. Msemaji wao, Sajbullah Mudjahid, alitangaza kwamba raia hao
wa kigeni walikuwa wanafanya ujasusi kwa niaba ya Marekani na
kuwabadilisha watu dini kwa ajili ya Ukrito. Mkuu wa polisi katika
mkoa wa Badakhshan, Jenerali Agha Nur Kemtus, amesema
yawezekana kwamba kisa hicho ni cha wizi wa kawaida bila ya
kushiriki Wataliban. Shambulio hilo lilifanyika Ijumaa iliopita.
Serekali ya Ujerumani imelaani vikali kushambuliwa raia wa kigeni
wanaotoa misaada huko Aghanistan. Serekali ya Ujerumani imetaka
ipatiwe maelezo ya kina juu ya mauaji hayo ya woga na waadhibiwe
wale waliofanya uhalifu huo. Hayo yalisemwa na naibu wa msemaji
wa serekali ya Ujerumani, Sabine Heimbach. Alisema kisa hicho
kinasisitiza juu ya umuhimu wa kusonga mbele katika kuchangia
kuleta utulivu katika Afghanistan. Pia chama cha Kijani na kile cha
die Linke vimekasirishwa na kisa hicho. Mkuu wa wabunge wa
Chama cha Kijani, Jürgen Trittin, amesema kuuliwa kwa wasaidizi
hao kunaonesha vipi Afghanistan ilivyo mbali kuwa nchi ilio tulivu.
Mkuu wa chama cha die Linke, Gesine Lötsch, kwa mara nyingine
tena, alitaka jeshi la Ujerumani liondoke kwa haraka kutoka
Afghanistan.