1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji mengine Tana River Kenya

21 Desemba 2012

Mapigano mapya yamezuka katika eneo la Tana River Kaskazini mwa ukanda wa Pwani nchini Kenya, ambako hadi kufikia sasa watu 39 wameripotiwa kufariki, ikiwa ni miezi michache tu baada ya ghasia nyengine kuua watu 100.

https://p.dw.com/p/177eX
Tana River Kenya.
Tana River Kenya.Picha: dapd

Majeruhi wakivukishwa kwa kutumia ngalawa kutoka eneo la Kipau ngambo ya pili ya Mto Odha kulikotokea mashambulio mwendo wa saa 12:00 alfajiri.

Hadi kukienda mitamboni, jumla ya majeruhi 25 walikuwa wamevukishwa mto huo na kusafirishwa hadi Hospitali ya Mji wa Malindi umbali wa kilomita 200 kutoka eneo la tukio.

Wavamizi hao wapatao 100 kutoka jamii ya Pokomo yadaiwa walivuka mto huo kutoka kijiji cha Ngao na kuwashambulia watu wa jamii ya Orma kwa mapanga na mishale katika kijiji hicho cha Kipau. Zaidi ya nyumba 47 pia zilichomwa moto wakati wa mashambulizi hayo ya alfajiri.

Katika kichaka kimoja kilichoko nje kidogo tu ya kijiji cha Kipau, mwanamke mmoja alikutikana amefariki baada ya kuvuja damu kupita kiasi kutokana na majeraha ya mapanga, kando yake akiwa moto wa umri wa miezi tisa.

Wengi ni wanawake na watoto

Maafisa wa Msalaba Mwekundu nchini Kenya wanasema kuwa wengi wa waliofariki walipoteza maisha yao katika mazingira hayo ya kuvuja damu kupita kiasia baada ya kukosa matibabu ya dharura.

Kijiji cha Shirikisho kilipovamiwa na kuteketezwa mwezi Septemba 2012.
Kijiji cha Shirikisho kilipovamiwa na kuteketezwa mwezi Septemba 2012.Picha: dapd

Miongoni mwa waliouawa wakati wa mashambulizi hayo ni watoto 13, wanawake sita wanaume 11 pamoja na wavamizi tisa. Hata hivyo maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya wanasema kuwa idadi hii huenda ikaongezeka kwani juhudi za kuwatafuta majeruhi waliotorekea vichakani bado inaendelea.

Hospitali kuu ya wilaya ya Malindi ilikuwa na shughuli nyingi na wakati mmoja kuonekana kushindwa kukabiliana na idadi ya marejuhi.

Mauaji haya yanatokea hatua chache tu kutoka eneo la Kilelengwani ambako zaidi ya watu 100, mifugo 400 na nyumba kuchomwa moto mwezi Agosti mwaka huu.

Wenyeji wa eneo hilo wanainyoshea kidole serikali na viongozi wa siasa kwa kile wanachokitaja kuwa mauaji ya halaiki.

Bado ya Agosti hayajasuluhishwa

Kufuatia mauaji ya mwezi Agosti, serikali ya Rais Mwai Kibaki ilipeleka vikosi vya jeshi la polisi na kutangaza amri ya kutotoka nje katika eneo hilo ambayo wenyeji wanasema kuwa ilidumishwa kwa muda mfupi.

Wanawake na watoto wakikimbia mauaji kwenye kijiji cha Oda, Tana River, mwezi Septemba 2012.
Wanawake na watoto wakikimbia mauaji kwenye kijiji cha Oda, Tana River, mwezi Septemba 2012.Picha: dapd

Aidha serikali ya Rais Mwai Kibaki pia ikateua tume ya kuchunguza mauaji hayo ya mwezi Agosti ikiongozwa na Jaji Grace Nzoika na hadi kufikia sasa haijakamilisha na kutoa ripoti yake kuhusiana na mauaji hayo ya Tana River.

Saumu Mwasimba amezungumza na msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya ambalo limekita kambi katika eneo hilo, Nelly Muluka, kuhusiana na hali ilivyo.

Kusikiliza mahojiano hayo, tafadhali bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini.

Mwandishi: Eric Ponda/DW Mombasa
Mhariri: Josephat Charo