Matumizi ya silaha za sumu Syria kuchunguzwa
5 Aprili 2017Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gueterres amesema mashambulizi yanayotuhumiwa kuwa ya silaha za sumu nchini Syria yanapaswa kuchunguzwa. Mohamed Dahman na taarifa kamili juu ya mashambulizi hayo ambayo yametokea hapo jana na kulaaniwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linatazamiwa kulijadili suala hilo katika kikao chake huko New York.
Kauli ya Guterres inakuja wakati kundi linalofuatilia hali ya Syria likisema idadi ya vifo kutokana na mashambulio hayo ya Jumanne katika mji wa kaskazini imeongezeka na kufikia 72, na wanaharakati pia wameripoti kurudiwa kwa mashambulizi ya anga katika mji huo.
Guteress amewaambia waandishi wa habari leo hii katika mkutano wa wafadhili wa Syria unaofanyika Brusels kwamba anataraji wakati huu utaweza kuimarisha uwezo wa wale ambao wana wajibu katika hali hiyo.
Amesema matukio hayo ya kutisha yanaonyesha uhalifu wa kivita ukiendelea kutendeka nchini Syria na kwamba sheria ya kimataifa inaendelea kukiukwa mara kwa mara.Ameongeza kusema ana imani kwamba Baraza la Usalama litatimiza wajibu wake wakati litakapokutana baadae leo hii.
Baraza la Usalama kujadili mashambulizi hayo
Marekani, Ufaransa na Uingereza zimewasilisha rasimu ya azimio kwa Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa likishutumu mashambulizi yanayotuhumiwa kuwa ya silaha za sumu hapo Jumanne katika mji unaoshikiliwa na waasi kaskazini magharibi ya Syria na kudai yafanyiwe uchunguzi.
Azimio la kurasa mbili ambalo shirika la habari la Ujerumani dpa lilipata nakala yake limetaka lipatiwe taarifa za kina juu ya operesheni za anga za ndege za jeshi la Syria na majina ya marubani wa helikopta za serikali. Shirika la Kupiga Marufuku Matumizi ya Silaha za Sumu limetaka lipatiwe nafasi ya kuzuru viwanja vya ndege vya kijeshi ambapo inadaiwa silaha hizo za sumu zilifyatuliwa.
Limetaka kukutana na majenerali wa Syria na viongozi wa Syria katika kipindi kisichozidi siku tano. Akizungumza hapo jana katika mkutano na waandishi wa habari msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujaric amesema Umoja wa Mataifa haukuthibitisha repoti za kutumika kwa silaha za sumu nchini Syria.
Utawala wa Assad umekuwa ukituhumiwa kutumia silaha za sumu mara kadhaa tokea vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza mwaka 2011 yakiwemo mashambulizi katika eneo la Ghouta karibu na mji mkuu wa Damascus kwa kutumia kemikali ya sumu ya sarin ambapo zaidi ya watu 1,400 walikufa katika shambulio la mwaka 2013.
Utawala wa Assad na silaha za sumu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson, amesema kwamba ushahidi wote wa mashambulio hayo ya sumu hadi sasa unaashiria kwamba ni serikali ya Assad iliyotenda hayo kwa kutambuwa fika kwamba inatumia silaha zilizopigwa marufuku kwa mashambulizi hayo ya kinyama dhidi ya wanachi wake wenyewe.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema wakaazi wa mji huo unaoshikiliwa na waasi wameathirika kutokana na kushambuliwa kwa kiwanda cha silaha za sumu cha waasi.Nchi zote mbili, Urusi na Syria, zimekanusha kufanya mashambulizi ya silaha za sumu.
Wafadhili wa kimataifa wanatafuta michango ya mabilioni ya dola kuisaidia Syria, nchi iliyoathirika na vita.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/
Mhariri: Mohammed Khelef