Matumaini yadidimia kuwapata waliotoweka katika vita Kosovo
15 Desemba 2021Bajram Cerkini mwenye umri wa miaka 82 ambaye anatoka katika jamii ya Albania na ambaye kijana wake Reshat ni miongoni mwa wale waliotoweka wasijulikane waliko hadi leo, anasema makovu ya vita hivyo ni donda dugu lisilopona akilini mwao. Anasema kila mara mke wake husikia sauti za mwanaye huyo usiku na kumhisi kana kwamba anatembea.
Vita hivyo vya mwisho wa miaka ya 1990 baina ya vikosi vya Serbia na wapiganaji wa jamii ya Albania vilisababisha vifo vya takriban watu 13,000. Na vilimalizika tu baada ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuingilia kati.
Maelfu ya watu walitoweka wasijulikane waliko hadi leo.
Baadhi yao walitekwa wakati wa maangamizi ya kikabila, miili yao ikazikwa katika makaburi ya pamoja, kuchomwa au kutupwa kwenye visima vya maji.
Miaka iliyofuata baada ya vita kumalizika, wataalamu wa uchunguzi kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni waliwasili Kosovo kufanya uchunguzi wa miili iliyopatikana ili kuwapa jamaa zao kwa mazishi, lakini vilevile kunakili mambo hayo kwa minajili ya uwezekano wa kufungua kesi ya uhalifu wa kivita dhidi ya wahusika.
Katika baadhi ya visa, vipande vidogovidogo vya mifupa ndivyo vilipatikana na kukabidhiwa familia.
Kulingana na maafisa wa Kosovo jumla ya watu 1, 625 hawajapatikana.
Mvutano kati ya Kosovo na Serbia
Hatma ya watu wasiojulikana waliko ni mojawapo ya masuala tete kati ya Kosovo na Serbia tangu mwaka wa 2008 wakati ambapo mpaka huo uliojitenga ulijitangazia uhuru wake. Tangazo ambalo Serbia haikuwahi kutambua rasmi.
Katika kipindi cha mwisho cha mapigano hayo kufuatia mashambulizi ya mabomu kutoka kwa NATO, vikosi vya Serbia vilijiondoa Kosovo. Makaburi ya Pamoja yalifukuliwa na miili kujazwa kwenye malori na kupelekwa Serbia ili kuficha Ushahidi wa uhalifu wa kivita.
Tangu vita hivyo kumalizika, takriban miili 1,000 ya watu wa jamii ya Albania kutoka Kosovo imefukuliwa katika makaburi mawili nchini Serbia, likiwemo kaburi moja karibu na kituo cha polisi viungani mwa mji wa Belgrade lililokuwa na mamia ya miili.
Andin Hoti ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya watu ambao hawajulikani waliko Kosovo na ambaye baba yake ni miongoni mwa wale wasiojulikana waliko, amesema kadri Waserbia walivyojaribu kuficha uhalifu ndivyo walivyofanya uhalifu zaidi.
Juhudi za kutafuta makaburi ya wakati wa vita
Masuala kama hayo yameikumba pia nchi jirani ya Bosnia ambako wataalam wangali wanajaribu kutambua makaburi ya pamoja karibu na Srebrenica ambako takriban wanaume 8,000 waumini wa Kiislamu 8,000 pamoja na vijana waliuawa na vikosi vya Serbia.
Almasa Salihovic ambaye ni msemaji wa kituo kimoja cha kimakumbusho ya Srebrenica amesema wangali wanatafuta zaidi ya watu 1,000 na kwamba hali inazidi kuwa ngumu kutambua mahali yaliko makaburi ya halaiki.
Nchini Kosovo suala la watu wasiojulikana waliko huwagusa raia kuliko hata siasa.
Katika mji mkuu Pristina maonesho ya kisanaa kwa jina ‘Kaburi ni bora kuliko kutojua aliko mtu wako‘, huelezea huzuni na machungu kutokana na suala hilo ambalo halijapata ufumbuzi.
Kwenye maonesho hayo, taa zinazowaka kwa muundo wa saa huonesha jumla ya saa na dakika ambazo zimepita tangu familia hizo kuwaona wapendwa wao mwisho.
Msanii aliyeyaunda maonesho hayo Driton Selmani amesema jamaa hawataki kufa kabla kujua ni wapi haswa wapendwa wao waliouawa walizikwa.
(AFPE)