Matumaini mapya Zimbabwe
23 Desemba 2009Taarifa iliyotolewa kufuatia mkutano wa Jumatatu kati ya Rais Mugabe na Waziri Mkuu Tsvangirai imesema kuwa viongozi hao wamewateua wajumbe wa Halmashauri ya Vyombo vya Habari, Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe na Halmashauri ya Haki za Binadamu ya Zimbabwe. Halmashauri hizo mpya zinatazamiwa kuleta mageuzi yaliyo muhimu sana kuvutia misaada ya kigeni. Wadadisi wanasema, uamuzi wa kuunda tume hizo mpya unatia moyo. Lakini mchambuzi Barnabas Thondlana anatanguliza mbele ukweli wa hali ya mambo.Anasema:
"Tunachohitaji ni kuimarisha taasisi na sio mtu mmoja mmoja. Watu hao wanaweza kubadilishwa lakini taasisi baadae huenda zikaendelea kuwa na matatizo."
Licha ya kuteuliwa kwa wajumbe wa halmshauri hizo tatu mpya, bado kuna masuala mengine ya utata. Kwa mfano Mugabe anakataa kumuapisha Roy Bennet kama makamu wa waziri wa kilimo.Bennet ni mshirika mwandamizi wa Tsvangirai na anakabiliwa na mashtaka ya uhaini. Vile vile Mugabe anakataa kuwafukuza kazi washirika wake wawili aliewateua kuiongoza Benki Kuu na kushika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu.
Katika mwezi wa Oktoba,Tsvangirai wa chama cha MDC alitangaza kuwa anajitoa katika serikali ya umoja wa kitaifa kwa sababu ya kutoweza kuafikiana kuhusu mada hizo. Chama cha ZANU-PF cha Mugabe kilipewa muda, hadi Januari 15 kuafikiana katika masuala hayo yote. Lakini majuma matatu baadae, Tsvangirai alirejea kufuatia jitahada za upatanishi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC- zilizoomgozwa na nchi jirani Afrika Kusini. Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alieleza hivi:
"Lilikuwa suala gumu sana. Tulizungumza na ndugu zetu wa Zimbabwe. Nadhani wameashiria kuwa wapo tayari kuhakikisha kuwa makubaliano yao yatatekelezwa. Kwa maoni yangu, sote tunapaswa kuwaunga mkono."
Makubaliano yaliyopatikana juma hili kati ya mahasimu Mugabe na Tsvangirai huenda ikawa ni hatua ndogo ya kwanza inayotoa matumaini kuwa serikali ya umoja wa kitaifa itadumu licha ya Rais Mugabe hivi karibuni tu kutamka kuwa serikali hiyo haina muda mrefu hivyo.
Mwandishi:Genthe,Jana/ZPR/P.Martin/RTRE
Mhariri: Miraji,Othman