Matukio muhimu katika miaka 50 ya Umoja wa Afrika
Wakati Umoja wa nchi Huru za Afrika (OAU) ukianzishwa Mei 25, 1963, viongozi wote 30 wa mataifa yaliyokuwa huru wakati huo walikuwepo. Muungano wa kisiasa ulipaswa kuzuia kugawanyika kwa bara la Afrika.
Mwanamke ulingoni
Mwaka 2012 Nkosazana Dlamini-Zuma alichaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Halmashauri ya Afrika, ambayo ndiyo ofisi ya juu kabisaa katika Umoja wa Afrika (AU). Waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani wa Afrika Kusini alileta sauti mpya katika Umoja wa Afrika, kwa mujibu wa waangalizi waliotoa maoni yao kuhusu siku zake mia moja za kwanza ofisini.
Muungano dhidi ya mgawanyiko
Wakati Umoja wa nchi huru za Afrika OAU ukianzishwa mnano tarehe 25 Mei 1963, mataifa yote 30 huru wakati huo yalikuwepo. Muungano huo wa kisiasa ulilenga kuzuia mgawanyiko wa bara la Afrika, kwa sababu chini ya ushawishi wa mataifa makubwa, makundi ya kupinga ukoloni yaligawanyika kati ya yanayounga mkono, na kupinga nchi za magharibi. Hii hapa ni picha ya mkutano mkuu wa OAU mwaka 1966.
Waanzilishi wa Umoja wa Afrika
Kwame Nkrumah (kushoto), rais wa kwanza wa Ghana na mfalme wa Ethiopia Haile Selassie (katikati) walikuwa miongoni mwa waasisi wa OAU. Nkruma alitoa pendekezo la kuwa na shirikisho la mataifa ya Afrika, ili kushindana na mataifa ya kikoloni, na kujenga soko la pamoja. Lakini mataifa hayo machanga wakati huo hayakuwa tayari kwenda umbali huo.
Adui wa pamoja
Malengo muhimu ya kisiasa ya Umoja wa nchi huru za Afrika katika miaka yake ya kwanza yalihusisha mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Katika mwaka wake wa kwanza, OAU iliunda kamati ya uhuru, na kuanzia mwaka 1970, iliunga mkono mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini.
Msukumo mpya wa kiuchumi
Kupitia Mpango wa Lagos wa mwaka 1980, OAU ililenga kukuza uchumi wa Afrika. Mpango huo ulijumuisha miongoni mwa mambo mengine uundwaji wa soko la pamoja kufikia mwaka 2000. Lakini kama ilivyo kwa mipango mingi ya kiafrika, mpango huo ulibaki tu katika maandishi. Mwaka 1991 ulifuatia mkataba wa Abuja, ambao uliweka lengo la kuanzishwa kwa jumuiya ya kiuchumi ya Afrika ifikapo mwaka 2025.
Sera ya ukombozi wa kijeshi
Licha ya kanuni zake kwamba hali ya mipaka inabaki bila kuguswa, OAU iliitambua Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahara (Sahara Magharibi), iliyotangazwa na Chama cha Polisario. Hii ilipelekea nchi ya Morokko kujitoa katika umoja huo, na hadi wakati huu, imeendelea kuwa nchi pekee ya kiafrika iliyojitoa katika umoja huo kwa hiari.
Ukosoaji wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika
Lakini Sahara Magharibi imeendelea kuwa mfano wa pekee wa mtazamo wa kisiasa wa OAU. Kwa sababu walitumia sera yao ya kutoingilia kati mfululizo, na hata wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda OAU ilikaa tu na kutazama. Hii iliwafanya wasomi kuuona umoja huo kama klabu ya madikteta. Moja wa wakosoaji wakubwa alikuwa rais wa Uganda Yoweri Museveni, aliechukua madaraka mwaka 1986.
Majeshi yasiyopendwa
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, OAU ilikuja na sera mpya: Afrika ilitaka kushughulikia migogoro yake yenyewe. Hii ilipelekea kuanzishwa kwa utaratibu wa amani. Yalipofanyika mapinduzi nchini Burundi mwaka 1996, OAU ilichukua hatua kwa kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Kwa ujumla utaratibu huo umeendelea kuwepo lakini una udhaifu mkubwa sana na moja ya sababu ni kutokana na umoja huo kukosa fedha .
Ushindi wa taratibu na endelevu
Sherehe kubwa za OAU zilifanyika mwaka 1994 wakati wa kuikaribisha Afrika Kusini katika umoja huo, miaka 30 baada ya kuanzishwa kwake. Kwa kuzingatia mchango unaotolewa na Afrika Kusini mjini Addis Ababa - kwa baadhi sherehe hiyo ilikuwa na umuhimu wa kipekee.
Mwanzo wa enzi mpya
Baada ya kumalizika kwa Vita Baridi na kukombolewa kwa Afrika Kusini, OAU ilianza kutafuta mwanzo mpya mwaka 1999. Hii ilitoa fursa kwa kiongozi wa Libya Muammar Ghaddafi (hapa akiwa katika mkutano mwaka 2007) , kuja na wazo la kuileta Afrika pamoja. Ili kufikia lengo hili, Ghaddafi alitumia utajiri wa nchi yake, kulipia madeni ya mataifa mengine.
Kutoka OAU hadi AU
Lakini Gaddafi hafanikiwa. Badala yake mpango wake ulizusha mgawanyiko zaidi baada ya kubadilisha kutoka Umoja wa nchi Huru za Afrika (OAU) kwenda Umoja wa Afrika (AU), huko mjini Durban Afrika Kusini mwaka 2002, ambapo yalijitokeza makundi yanayounga mkono na kumpinga. Muongozo wa kuanzishwa kwa AU uliondoa sera ya zamani ya kutoingilia kati masuala ya nchi. Hapa ni picha ya uzinduzi wa AU.
Taasisi isiyo na nguvu
AU ilichukua ruwaza ya Umoja wa Ulaya kama muundo wake wakati ikianzishwa, na pia iliona umuhimu wa kuwa na bunge la Afrika. Bunge hilo lilianzishwa mwaka 2004 likiwa na wajumbe 235 kutoka mataifa 47. Makao ya bunge hilo yaliwekwa nchini Afrika Kusini katika mji wa Midrand. Umbali wa bunge hilo kutoka makao makuu ya AU mjini Addisa Ababa unaonyesha ushawishi wa kisiasa wa chombo hicho kidogo.
Ushiriki mpya katika kuleta amani
Mwanzoni mwa karne mpya, asilimia 20 ya wakaazi wa Afrika walikuwa wameathiriwa na vurugu zinazotokana na migogoro. Hivyo amani ilikuwa suala muhimu kwa Umoja wa Afrika, na mwaka 2004 umoja huo uliunda baraza la amani na usalama, ambalo lilipewa jukumu la kuunda kikosi cha kuingilia kati migogoro. Katika mwaka huo, baraza hilo lilituma wanajeshi kulinda raia katika jimbo la Darfur nchini Sudan.