Matokeo ya uchaguzi Zimbabwe kutatangazwa usiku
2 Agosti 2018Ghasia zilizofuatia uchaguzi zilisababisha umwagikaji wa damu, siku moja baada ya kuushutumu upinzani kuwa unachochea vurugu. Hivi sasa polisi imeyafunga makao makuu ya chama cha upinzani cha MDC mjini Harare.
Wanajeshi wamewaondoa watu kutoka mitaa ya eneo la kati la mji wa Harare mji mkuu wa Zimbabwe baada ya kutumia risasi jana kuwatawanya waandamanaji ambao wamekasirishwa kuhusiana na madai ya udanganyifu katika uchaguzi uliofanyika kwa amani siku ya Jumatatu, uchaguzi wa kwanza ambao umefanyika bila ya kiongozi wa siku nyingi Robert Mugabe kugombea.
Jumuiya ya madola, Commonwealth imejiunga na waangalizi wengine wa uchaguzi katika kuitaka Zimbabwe kutoa matokeo ya kiti cha urais haraka iwezekanavyo ili kupunguza hali ya wasi wasi , ikisema kuendelea kuchelewesha matokeo kutaongeza uvumi kwamba matokeo yanachakachuliwa. Tume ya uchaguzi imesema matokeo yatatolewa hivi karibuni.
Katika maandishi kadhaa katika ukurasa wa Twitter, rais Emmerson Mnangagwa amesema "tunawasiliana na mgombe wa upinzani Nelson Chamisa na kwamba "tunapaswa kuendeleza majadiano ili kulinda amani yetu muhimu." Katibu wa chama tawala cha ZANU-PF anayehusika na masuala ya kisheria Paul Mangwana amesema matukio yaliyotokea jana yanasikitisha.
"Kutokana na matukio yaliyotokea jana, ni masikitiko makubwa kwamba watu walipoteza maisha. Tunatoa pole kwa wale wote waliopoteza ndugu zao. Tulifanya uchaguzi wetu katika mazingira ya amani. Na tuna matumaini kwamba hali hiyo itaendelea hadi yatakapotangazwa matokeo. Tunatoa wito kwa wenzetu wa upinzani kuhakikisha kwamba waungaji wao mkono , wanaendeleza utulivu uliokuwapo wakati wa kupiga kura.
Maridhiano
Matamshi hayo ya maridhiano yanakuja siku moja baada ya wanajeshi kutumia risasi za moto na kuwapiga waandamanaji , wengi wao walikuwa wakirusha mawe na kuwasha moto wakipinga madai ya udanganyifu katika uchaguzi huo. Serikali imesema watu watatu wameuwawa. Tume ya uchaguzi pia imetoa taarifa ya kushutumu vikali matukio ya jana.
"Tume inapenda pia kusema kwamba inashutumu vikali matukio ya jana, matukio haya ambayo yamesababisha watu kupoteza maisha yanasikitisha na yangeweza kuepukwa. Tume inatoa pole kwa fmilia za waliofariki na wale ambao wamejeruhiwa, na tunawatakia wale waliojeruhiwa kupona haraka."
Polisi ya Zimbabwe imefunga makao makuu ya chama cha upinzani Movement for Democratic Change MDC na wafanyakazi 27 wa chama waliokuwa wanajumlisha hesabu za kura wamefungiwa ndani, katibu mkuu Douglas Mwonzora alisema leo. Hali kwa mujibu wa mkaazi mmoja wa mji wa Harare Paul tawanda ni shwari.
"Leo ni shwari, maduka yote yamefungwa kwasababu hali ni ya wasi wasi kwamba ghasia zinaweza kuanza tena leo. Lakini amani imeendelea kuwapo , polisi wamerejesha amani , lakini watu wengi wamekwenda nyumbani, walikuja kazini, lakini wamerejea nyumbani kwasabahu ofisi zimefungwa."
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres ameeleza wasi wasi wake kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi nchini Zimbabwe. Guterres amewataka viongozi wa kisiasa na umma kwa jumla kuvumiliana na kukataa kila aina ya ghasia wakati wanasubiri matokeo kutangazwa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape rtre
Mhariri: Josephat Charo