1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zimbabwe, yaanza kutolewa baada ya kucheleweshwa.

Nyanza, Halima31 Machi 2008

Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe imeanza kutoa matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Jumamosi, baada ya kulalamikiwa kuchelewa kutokana na madai ya kutaka kumsaidia Rais Robert Mugabe aweze kuongoza tena.

https://p.dw.com/p/DXlb
Wananchi wa Zimbnabwe wakiangalia matokeo ya uchaguzi mkuu, yaliyobandikwa ubaoni, baada ya kupiga kura siku ya Jumamosi.Picha: AP

Matokeo hayo yameanza kutangazwa na Tume hiyo ya uchaguzi huku upinzani nchini humo, wakidai kushinda katika uchaguzi huo, hali ambayo wanadai ndio sababu iliyofanya matokeo kuchelewa, ili kuweza kutoa nafasi kwa hila kufanyika kuweza kumpa ushindi Rais Mugabe, ambao wamedai kuwa ameshindwa katika uchaguzi huo.

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, kimedai kupata matokeo mazuri zaidi, kumshinda Rais Mugabe ambaye ndiye anayetetea kiti chake, huku vikosi vya jeshi vikiwa vimezagaa mitaani leo.

Mapema leo asubuhi, Naibu Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo Utoile Silaigwana alitangaza matokeo ya viti 12 vya bunge ambapo 12 vilikuwa vimechukuliwa na chama cha Rais Mugabe na Vingine 12 vilikwenda kwa upinzani.

Hata hivyo wasimamizi wa uchaguzi ambao hawakutaka kutajwa majina yao kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kutangaza matokeo, wamesema mawaziri sita wamepoteza nafasi zao bungeni.

Wakati polisi wa kutuliza ghasia wakiwa wametawanywa katika mitaa ya jiji la Harare, chama cha Rais Mugabe cha ZANU PF na kile cha upinzani cha Movement for Democratic change MDC, vimekuwa vikikabiliana kwa karibu kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo ya ya awali ambapo viti 24 kati ya viti 210 vya bunge vilitangazwa, huku Waziri wa Sheria wa nchi hiyo Patrick Chinamasa akipoteza kiti chake.

Chama cha upinzani cha MDC kilishinda kiti cha kwanza kutangazwa, huku wafuasi wake wakishangilia ushindi huo wa awali wakiamini kuwa watapata ushindi wa jumla.

Kiongozi wa upinzani wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai amekuwa na matumaini ya kumuondoa madarakani Rais Mugabe katika uchaguzi huu, ambapo chama chake jana kiliilaumu tume ya uchaguzi nchini humo, kwa kutotangaza kwa wakati matokeo hayo baada ya uchaguzi wa Jumamosi kwa madai kuwa inampangia ushindi Rais Mugabe ambaye ameongoza nchi hiyo toka ilipopata uhuru wake mwaka 1980 .

Katibu Mkuu wa chama hicho cha MDC Tendai Biti alitamka wazi kwamba Rais Mugabe ameshindwa katika uchaguzi huo na hivyo tume imekuwa ikijaribu kutengeneza matokeo yatakayompa ushindi, hivyo chama chao hakitakubali hali hiyo.

Kutokana na kuhofia kuzuka kwa ghasia kama zile zilizotokea nchini Kenya baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa nchi hiyo na kusababisha vifo vya zaidsi ya watu elfu moja, vyombo vya ulinzi nchi ni Zimbabwe vimewekwa katika hali ya tahadhari, huku polisi wa kutuliza ghasia wakifanya doria mitaani.

Mbali na Rais Mugabe kupata upinzani kutoka kwa Morgan Changirai, katika uchaguzi wa mwaka huu pia anapata changamoto kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Simba Makoni, ambaye binafsi alisema pia anafuatilia kwa makini yote yanayojiri katika zoezi hilo la uchaguzi.

Amefafanua kuwa atasubiri mpaka matokeo yatakapotoka, halafu kuyalinganisha kutokana na mazingira yaliyokuwapo, na baadaye kutoa msimamo wao.

Uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe umefanyika huku kukiwa hakuna waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya ama Marekani walioruhusiwa wakati wa zoezi hilo.

Uchaguzi huo pia umefanyika wakati nchi hiyo ikikabiliwa na matatizo makubwa kiuchumi.

Rais Mugabe amekuwa akilaumu matatizo ya uchumi nchini humo kwamba yanasababishwa na na Umoja wa Ulaya na Marekani ambazo zimeiwekea vikwazo nchi hiyo kwa madai ya kufanya hila katika uchaguzi wa mwaka 2002.