Matokeo ya uchaguzi mkuu bado yasubiriwa Tanzania
3 Novemba 2010Chama tawala nchini Tanzania CCM kimesema kinataraji kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais na wa bunge uliofanyika Jumapili iliyopita nchini humo. Hata hivyo waangalizi wa kimataifa wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na utaratibu wa kuhesabu kura. Kwa siku ya pili polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wanalalamikia kucheleweshwa kutolewa kwa matokeo mjini Dar es Salaam na katika maeneo mengine nchini Tanzania.
Mapema, mgombea wa urais aliyeshindwa Visiwani Zanzibar, Seif Sharif Hamad, alisema uchaguzi huo ulikuwa na walakin lakini akakubali atachukua wadhfa katika serikali ya muungano visiwani humo ili kuzuia machafuko yaliyotokea katika chaguzi mbili zilizopita visiwani Zanzibar.
Kiongozi wa kundi la waangalizi wa Umoja wa Ulaya David Martin alisema walikuwa na wasiwasi kuhusiana na utaratibu wa kutolewa matokeo. Hata hivyo mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya uchaguzi nchini Tanzania Lewis Makame ameondoa wasiwasi akisema hadi kesho matokeo yote yatakuwa yametolewa.
Meneja wa Kampeni wa CCM Abdulrahman Kinana amesema wanatarajia kupoteza viti 51 kwa upinzani lakini hawana shaka watashinda uchaguzi.