Matokeo ya michuano ya Kombe la FA Uingereza
5 Januari 2015Ni Queens Park Rangers pekee iliyoshindwa kuhimili vishindo. QPR ilipokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Sheffield United, ambayo imekuwa na tabia sasa ya kuviangusha vigogo katika mashindano ya kuwania vikombe..
Manchester City ilionekana kuelekea kuadhirika kama QPR, hadi pale James Milner , mchezaji wa kati ambaye alipangwa siku hiyo kucheza kama mshambuliaji kufunga mabao yote mawili ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sheffield Wednesday. Manchester United pia haikuonekana kuwa tishio dhidi ya timu ya daraja la tatu ya Yeovil na kupata ushindi wa taabu wa mabao 2-0.
Chelsea pia ilihitaji hadi kipindi cha pili kuweza kuwazidi nguvu wapinzani wake baada ya kufunga mabao 3 katika kipindi cha dakika 14 na kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Watford.
Arsenal ilipata kidogo afueni , baada ya mabingwa hao watetezi wa kombe hilo kupachika mabao 2-0 dhidi ya Hull City inayocheza katika ligi kuu pia.
Wakati huo huo kocha wa Arsenal , Arsene Wenger anaamini kuwa kiwango anachoonesha mshambuliaji wake Alexis Sanchez kwa kucheza bila kuchoka , inathibitisha kuwa mshambuliaji huyo kutoka Chile ana stamina ya kutosha kukiongoza kikosi cha washika bunduki hao katika changamoto ya kuwania vikombe msimu huu. Kocha wa Manchester City Manuel Pellegrini amesema anataka mkataba wa James Milner utatuliwe haraka baada ya mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Uingereza kuivusha timu hiyo katika duru ya nne ya kombe la FA jana. Nae kocha wa Manchester United Louis van Gaal amesema kipindi cha sikukuu ya Chrismas kimekuwa cha ushindi kwa kikosi chake baada ya kuiangusha Yeovil Town katika ya duru ya nne ya kombe la FA jana Jumapili.
Nae kocha wa Chelsea Jose Mourinho amesema kikosi chake kina uwezo wa kupambana katika mashindano manne tofauti. Kocha huyo hata hivyo ameomba radhi kwa mwamuzi wa pambano la jana dhidi ya timu ya daraja la kwanza ya Watford, baada ya kumshutumu mwamuzi Kevin Friend. Mourinho alilalamika katika mahojiano katika televisheni kwamba kikosi chake kilistahili kupata penalti katika hatua za kuelekea katika kupata bao lake la pili wakati Craig Cathcart alionekana kuunawa mpira baada ya kuzuwia mkwaju wa Diego Costa.
Lakini mwamuzi Freind hata hivyo alimfafanulia Mourinho kwamba aliacha mchezo uendelee , hali iliyowezesha mshambuliaji Loic Remy kupachika bao muda mfupi baadaye, na kocha huyo raia wa Ureno alikiri baaadaye kuwa shutuma zake hazikuwa na maana.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre , afpe , dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga