Matokeo ya chaguzi katika nchi 5 za Afrika yaanza kutolewa
21 Machi 2016MPD kimeking'oa PAICV madarakani baada ya kuongoza Cape Verde kwa miaka kumi na tano. Matokeo ya uchaguzi wa Rais pia yanatarajiwa kutolewa rasmi Niger, Congo na visiwani Zanzibar katika chaguzi zilizofanyika barani Afrika siku ya Jumapili
Waziri mkuu wa Benin Lionel Zinsou ameliambia shirika la habari la AFP kuwa matokeo ya awali yanaashiria ushindi kwa Patrice Talon na hivyo amempigia simu Talon kumpongeza kwa kushinda katika uchaguzi, kumtakia kila la kheri na kumueleza anajiandaa kukabidhi madaraka.
Takriban wapiga kura milioni 4.7 walisajiliwa kushiriki katika uchaguzi huo wa Benin wa kumchagua rais mpya atakayechukua wadhifa huo baada ya Rais Thomas Boni Yayi kukamilisha mihula miwili madarakani kuambatana na katiba.
Talon ambwaga Zinsou Benin katika duru ya pili
Boni Yayi ni miongoni mwa viongozi wa Afrika ambao wameheshimu katiba za nchi zao kwa kutozifanyia marekebisho ili kusalia madarakani. Zinsou mwenye umri wa miaka 61 aliibuka mshindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais mnamo tarehe sita mwezi huu kwa asilimia 27.1 huku Talon alikuwa nafasi ya pili kwa asilimia 23.5.
Zinsou ambaye anaungwa mkono na Rais Boni Yayi alipigiwa upatu kushinda kwani alikuwa pia anaungwa mkono na wabunge wengi.
Lakini mpinzani wake Talon mwenye umri wa miaka 57 ambaye ni tajiri kutokana na biashara ya pamba na kuendesha biashara katika bandari ya Cotonou, amejinadi kama raia halisi wa Benin.
Nchini Cape Verde, chama kikuu cha upinzani MPD kimeshinda baada ya uchaguzi wa jana kwa zaidi ya asilimia 53 na mkuu wa chama tawala PAICV Janira Hopfer Almada amekubali kushindwa baada ya asilimia 90 ya matokeo kutangazwa.
Chama tawala Cape Verde chang'olewa madarakani
Kiongozi wa MPD Ulisses Correia e Silva amesema matokeo hayo yanaonyesha hamasa ya kweli ya kutaka mabadiliko katika taifa hilo na kuongeza kuna kazi nyingi ya kufanya kwa serikali mpya kwasababu nchi inahitaji ukuaji imara wa kiuchumi ili kutatua matatizo ya ukosefu wa ajira na kupunguza umaskini.
PAICV kinaondoka madarakani baada ya kuiongoza Cape Verde kwa miaka 15 iliyopita. MPD kimepata viti 36 vya bunge huku PAICV kikipata viti 25 na chama cha Christian Democratic UCID kikipata viti vitatu. Bunge la Cape Verde lina viti 72 kwa jumla.
Katika uchaguzi mwingine mkuu uliofanyika hapo jana, Rais wa Niger Mahamadou Issoufou anatarajiwa kushinda baada ya upinzani kuususia uchaguzi. Kiongozi wa upinzani Hama Amadou alisafirishwa nje ya nchi kwenda kupata matibabu wiki iliyopita.
Issoufou ambaye ni mshirika wa nchi za magharibi alishinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwezi uliopita kwa asilimia 48 lakini alishindwa kupata wingi wa kura kuepusha duru nyingine ya uchaguzi. Issofou amesema atakayeshinda atakuwa na kibarua cha kuwaunganisha raia wa nchi hiyo
Issofou na Sassou Ngueso wanatarajiwa kusalia madarakani
Katika Jamhuri ya Congo, Rais wa nchi hiyo wa muda mrefu Denis Sassou Nguesso naye anatarajiwa kusalia madarakani hata baada ya kuliongoza taifa hilo kwa miaka 32.
Vituo vya kupigia kura vilifungwa jana jioni na matokeo yanatarajiwa kutolewa hapo kesho. Waziri wa mambo ya ndani wa Congo Raymond Mboulu aliziamirisha kampuni za mawasiliano kuzima mawasiliano yote ya simu na mitandao kwa saa 48 kwasababu alizozaitaja za usalama wa kitaifa.
Na matokeo ya kura ya maoni nchini Senegal ya kufanyia marekebisho katiba ili kupunguza muda wa kuhudumu wa Rais kutoka miaka saba hadi mitano yanatarajiwa kutolewa leo.
Idadi ndogo ya wapiga kura ilijitokeza kushiriki katika kura hiyo ya maoni. Rais wa Senegal Macky Sall, aliahidi mwaka 2012 kupunguza muda wa kuhudumu wa rais.
Hata hivyo mahakama ya juu ya Senegal ilikataa pendekezo hilo mwezi uliopita na kusababisha kuitishwa kwa kura hiyo ya maoni. Iwapo kura ya ndiyo itashinda, Sall anatarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2019.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga