Matokeo ya awali ya Uchaguzi Afghanistan kutangazwa leo.
25 Agosti 2009Tuhuma zilianza kujitokeza miaka miwili kabla ya uchaguzi, baada ya Azizullah Lodin, mshauri wa zamani wa Rais wa nchi hiyo Hamid Karzai katika jimbo la Magharibi la Herat na msomi wa zamani kuteuliwa kuiongoza Tume huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo.
Uteuzi huo ulitangazwa Januari 3 mwaka 2007 na Rais Karzai kudharau wito uliotolewa na wanasiasa wa upinzani kwa Bwana Lodin kuidhinishwa na bunge.
Katika siku ya uchaguzi, Mkuu huyo wa Tume huru ya Uchaguzi alitoa taarifa za kuipongeza nchi, kwa wapiga kura wengi kujitokeza siku hiyo kupiga kura, licha ya ripoti zilizotolewa na Waangalizi huru wa uchaguzi kwamba ushiriki wa watu katika uchaguzi huo, ulikuwa ni mbaya kushinda mwengine wowote katika kumbukumbu za hivi karibuni.
Tume hiyo ya uchaguzi ilitabiri asilimia 50 ya watu waliojitokeza kupiga kura, huku waangalizi wa uchaguzi wakionesha ushiriki kuwa chini ya asilimia 10 katika baadhi ya sehemu zenye wafuasi wengi wa Taliban, mafanikio ambayo yanatia shaka hata katika uchaguzi wa kwanza ulioandaliwa na wa Afghanistan wenyewe tangu mwaka 2001 wakati wa uvamizi wa majeshi yanayoongozwa na Marekani.
Wakati Tume ya Uchaguzi ikitangaza matokeo hayo leo kwa mara ya kwanza, katika nchi hiyo ambayo imekuwa katika hali ya mashaka kisiasa tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Rais wiki iliyopita huku wagombea wawili wanaochuana vikali katika nafasi hiyo kila mmoja akidai ushindi na pia kuwepo kwa madai ya udanganyifu, jana jioni Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Hazrat Omar Zakhilwal alisema takwimu alizotumiwa zinaonesha kuwa Rais Hamid Karzai anaongoza kwa asilimia 68 ya kura zote zilizopigwa na kwamba amefanikiwa kuepuka kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi.
Naye msemaji wa mpinzani mkuu wa Rais Karzai, Abdullah Abdullah amesema takwimu hizo zote zilizotolewa ni za uongo.
Bwana Abdullah naye tayari alitangaza kushinda katika uchaguzi huo, huku akimlalamikia mpinzani wake kwa kufanya udanganyifu.
Akizungumzi kuhusiana na na malalamiko kuhusiana na uchaguzi yanayotolewa, Mkuu wa Tume Inayochunguza Malalamiko ya Uchaguzi Grant Kippen alikuwa na haya ya kusema.
Naye Msemaji wa Tume ya Uchaguzi Noor Mohammad Noor amesema karibu asilimia 10 ya matokeo yatatangazwa leo jioni.
Mwandishi: Halima Nyanza(AFP, Reuters)
Mhariri: M.Abdul-Rahman