Matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais Madagascar kutangazwa leo
8 Januari 2019Matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais yanatarajiwa kutangazwa leo nchini Madagascar baada ya Andry Rajoelina kutangazwa mshindi na wafuasi wa mpinzani wake kuandamana kupinga tangazo hilo.
Kulingana na matokeo kamili ya duru ya pili ya uchaguzi uliiofanyika tarehe 19 Desemba, Rajoelina alipata asilimia 55 ya kura huku Marc Ravalomanana akipata asilimia 44. Ravalomanana aliwasilisha kesi ya kupinga matokeo hayo katika mahakama ya kikatiba kwa madai ya kuwepo udanganyifu wa kura na mahakama hiyo inatarajiwa leo kumtangaza mshindi rasmi wa uchaguzi huo.
Wiki iliyopita, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya maelfu ya wafuasi wa Ravalomanana waliokuwa wakiandamana katika mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo.
Ravalomanana na Rajoelina wote wawili ni marais wa zamani wa taifa hilo ambao walizuiwa kuwania urais mwaka 2013 kama sehemu ya makubaliano ya kukomesha mizozo ambayo imeikumba Madagascar tangu ijinyakulie uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.
Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya na wa Umoja wa Afrika wamesema hawakuona ushahidi wowote wa udanganyifu wa kura.