1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka wote 22 wa Korea Kusini wangali hai

Josephat Charo27 Julai 2007

Msemaji wa kundi la Taliban nchini Afghanistan amesema mateka wote 22 wa Korea Kusini wako salama. Wakati huo huo, raia kadhaa wa Afghanistan wameuwawa kwenye mashambulio ya angani ya jeshi la NATO kusini mwa Afghanistan.

https://p.dw.com/p/CHAQ
Jamaa za mateka mjini Seoul
Jamaa za mateka mjini SeoulPicha: AP

Msemaji wa kundi la Taliban nchini Afghanistan, Qari Mohammed Yousuf, amethibitisha kwamba mateka wote 22 wa rehani raia wa Korea Kusini wangali hai. Aidha kiongozi huyo amesema mazungumzo yanaendelea baina ya kundi la Taliban na serikali ya mjini Kabul kujaribu kufikia makubaliano ya kuwaachilia huru mateka hao.

Kundi la Taliban halijaipa serikali ya rais Hamid Karzai muda itekeleze masharti iliyoyatoa, likisema limeahidiwa na serikali kuwa inataka kuumaliza mzozo huo kwa njia ya mazungumzo.

Kiongozi wa ujumbe wa Afghanistan kwenye mazungumzo ya kuwaokoa mateka wa Korea Kusini, Munir Mangal, pia amethibitisha kuwa mateka hao bado wangali hai. Amesema watafanya juhudi mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha mateka wote wanaachiwa kwa amani kupitia mazungumzo. Ikiwa njia zote zitashindwa, basi watachukua uamuzi mzuri utakaofaa.

Mke wa aliyekuwa kiongozi wa kundi la Wakorea Kusini 23 waliokuwa wakifanya kazi nchini Afghanistan kwenye mradi unaodhaminiwa na kanisa la Presbiteri mjini Seoul, amelitolea mwito kundi la Taliban mjini Seoul hii leo kulitaka liwaachilie huru mateka wote 22. Amesema ana matumaini uchungu wanaousikia Wakorea Kusini, kufuatia mumewe kuuwawa, hautaongezeka kwa mauaji mengine ya Wakorea nchini Afghanistan.

Sambamba na hayo, raia kadhaa wa Afghanistan wameuwawa kwenye mashambulio ya angali yaliyofanywa na jeshi la jumuiya ya NATO kusini mwa nchi hiyo. Shambulio moja lilizilenga nyumba katika wilaya ya Girishk mkoani Helmand na kuua raia takriban 50, wakiwemo wanawake na watoto.

Afisa wa jeshi la NATO aliyejitambulisha kwa jina Thomas amesema kuna uwezekano kuwa raia ni miongini mwa waliouwawa kwenye shambulio hilo.

´Kama mjuavyo hatujathibitisha lolote kwa kweli kufikia sasa. Lakini tujuavyo ni kuwa baada ya mapambano kusita, na baada ya kwenda kwenye eneo la mapigano, huenda kukawa na raia waliouwawa. Tumeona maiti zinazodhaniwa kuwa za raia miongoni mwa maiti za wanamgambo waliouwawa.´

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amekasirishwa sana na mauaji ya raia yaliyofanywa kwenye mashambulio ya angani ya jeshi la NATO. Amesema serikali yake inataka kushirikiana na jumuiya ya kimatiafa lakini maisha ya Waafghanistan sharti yaheshimiwe.

´Tunataka kushirikiana na jumuiya ya kimatiafa. Tunashukuru kwa msaada wake kwa Afghanistan. Lakini hiyo haina maana kwamba maisha ya Wafghanistan ni bure. Maisha ya Waafghanistan si bure na hayapaswi kuchukuliwa hivyo.´

Rais Karzai ameikosoa tabia ya wanajeshi kuyalenga maeneo yaliyo mbali kwa silaha. ´Hupigani na gaidi kwa kuvurumisha silaha kulenga aneo lililo umbali wa kilomita kadhaa kutoka mahala ulipo. Hatua hiyo bila shaka husababisha maafa kwa raia.´

Kufikia sasa rais Karzai hajasema lolote kuhusu kutekwa nyara mateka wa Korea Kusini lakini ameahidi kutowaachia wafungwa wa Taliban baada ya kukosolewa vikali kwa kufanya hivyo mnamo mwezi Machi mwaka huu ili kuyaokoa maisha ya mwandishi wa habari wa Italy.