Mateka wa Korea Kusini wameachiwa huru
31 Agosti 2007Mateka hao walitiririkwa na machozi wakati walipokutanishwa pamoja katika mahala pa siri mapema leo baada ya kuzuiliwa kwa wiki sita na wanamgambo wa Taliban.
Lakini licha ya pilikapilika za kutafuta kuachiliwa huru mateka hao 19 raia wa Korea Kusini waliokuwa wanazuiliwa na wanamgambo wa Taliban
wanasiasa wa nchini Afghanistan, Kanada na Ujerumani wameilaumu serikali ya Seoul kwa kujadiliana na wanamgambo hao wa Taliban.
Mateka hao waliokuwa wakifanya kazi ya kutoa misaada waliachiliwa kwa awamu kuanzia siku ya Jumatano na jana Alhamisi katika maeneo tafauti katikati ya jimbo la Ghazni nchini Afghanistan na kwa mshangao mkubwa ndipo wakatambua kwamba wawili kati ya wenzao waliotekwa nyara pamoja wameuwawa.
Wanamgambo wa Taliban wenye msimamo mkali waliwauwa mateka wawili kati ya mateka 23 waliowateka nyara tarehe19 mwezi Julai mmoja alikuwa ni mchungaji aliyekuwa na umri wa miaka 42 na wapili ni mmishionari aliyekuwa na umri wa miaka 29 baadae waliwaachia huru wanawake wawili na kuwabakisha mateka wengine 19 ambao kwa sasa wamewaachia huru.
Msemaji wa Kundi la Taliban Kari Yusuf Ahmadi wakati wa kuachiliwa kundi la mwisho la mateka saba raia Wakorea Kusini alisema mateka hao wana ujumbe kwa serikali yao ya Korea, jamii ya Wakorea na kwa vyombo vya habari.
Katika ujumbe huo Wataliban wanapinga Korea Kusini kushiriki kwenye vita dhidi ya ugaidi vinavyo ongozwa na Marekani na vile vile kuwatuma wamishionari nchini Afghanistan.
Msemaji katika ofisi ya rais nchini Afghanistan Homayun Hamidzada amesema kwamba serikali ya Afghanistan iliruhusu mazungumzo kati ya wawakilishi wa Korea Kusini na wanamgambo wa Taliban kwa sababu za kibinadamu lakini amekanusha kwamba serikali ya Afghanistan ilihusika katika mazungumzo hayo.
Msemaji huyo amefahamisha pia kwamba serikali ya Afghanistan inafanya kila jitihada za kuachiliwa mhandisi raia wa Ujerumani na raia wanne wa Afghanistan wanaozuiliwa na wanamgambo wa Taliban kwa zaidi ya wiki sita sasa.
Taarifa za hivi punde zinafahamisha kwamba mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejilipua kwa bomu karibu na uwanja wa ndege wa Kabul, askari mmoja imeripotiwa ameuwawa kwenye shambulio hilo.