1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Donald Trump na chuki dhidi ya waislam

9 Desemba 2015

Lawama dhidi ya matamshi ya chuki ya mgombea wa chama cha Republican cha Marekani, Donald Trump, sababu za kuenea siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya na mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi magazetini.

https://p.dw.com/p/1HJgx
Donald Trump,mgombea wa chama cha Republican-MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini matamshi yaliyotolewa na mgombea wa kiti cha rais wa Marekani,mrepublican Donald Trump.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten linasema:"Tatizo sio Trump" bali chama cha kimambo leo cha Republican ambacho neno,"taratibu" limegeuka kuwa tusi.Trump aliposhauri ujengwe ukuta wenye urefu wa maili 2000 katika mpaka wa Marekani na Mexico,watu walimpigia makofi.Hakuna pia aliyeudhika alipowatumbukiza katika kikapu kimoja raia wa Mexico na wabakaji na wauza madawa ya kulevya.Wachache tu ndio waliopinga pale Trump alipotishia kuwarejesha walikotokea wahamiaji milioni 10 wasiokuwa na vibali.

Donald Trump anatafuta mashaka

Mhariri wa gazeti la "Neue Westfällische" anahisi Donald Trump ananyunyizia mafuta katika cheche za moto.Anaendelea kuandika:"Pasiwe na yeyote atakaeshangaa pindi yakizuka mashambulio dhidi ya waislam nchini Marekani.Donlad Trump anapuliza tarumbeta na kupalilia hisia "inatosha sasa."Kwa kueneza fitina hizo,Donald Trump amejiondolea mwenyewe sifa ya kuwa mgombea mstahiki wa kiti cha rais wa Marekani. Chama cha Republican kinabidi kiwe na moyo wa kulitamka hilo hadharani.

Chanzo cha kuenea siasa kali za mrengo wa kulia Ulaya

Hisia za chuki dhidi ya wageni zinatishia pia kuenea barani Ulaya. Gazeti la Badische Zeitung linaandika:"Siasa kali za mrengo wa kulia zinapata nguvu barani Ulaya kwasababu watu wanahisi migogoro ya miaka iliyopita haijapatiwa ufumbuzi. Wananchi wengi wanasumbuliwa na migogoro ya kiuchumi nchini Ufaransa,kukwama shughuli za kiuchumi nchini Poland na uwezekano wa kushindwa sera za Umoja wa Ulaya nchini Ugiriki. Kinachohitajika ni matokeo bayana ya juhudi za kisiasa.

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi utamalizika kwa maridhiano au vipi?

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi unaoendelea Le Bourget karibu na Paris,nao pia umechambuliwa na wahariri wa magazeti. Landeszeitung linaandika: "Kila kitu kinaashiria kwamba mkutano wa mabadiliko ya tabianchi utamalizika kama ilivyomalizika mikutano mingi kabla ya huu. Baada ya majadiliano magumu na ya muda mrefu,watajitokeza watu mbele ya kamera wenye nyuso zilizochoka na kutangaza makubaliano yanayolingana na nyuso hizo; wakihoji" bora haya yaliyofikiwa kuliko kutofikiwa chochote."Hoja za kila aina zitatolewa ikiwa ni pamoja na masuala ya masilahi ya kiuchumi. Lakini suala hapa si la mustakbal wa kiuchumi,suala hapa linahusu mustakbal wa sayari ya dunia.

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef