1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ulaya yamekubali kuupiga jeki mfumo wa fedha.

Kalyango Siraj13 Oktoba 2008

Nayo Ujerumani itatoa Euro billion 400 kwa ajili hiyo

https://p.dw.com/p/FYQu
Kansela Angela Merkel.Picha: AP

Viongozi wa mataifa ya Ulaya yanayotumia sarafu ya Euro,mkiwemo Ujerumani wamekubaliana kuchukua hatua za kuupiga jeki mfumo wa fedha ili kuuepusha na mgogoro unaoendelea kwa sasa.

Ingawa Berlin haijafafanua mpango wake lakini wadadadisi wanasema unaweza ukafikia Euro billioni 400.

Kufutia mkutano wa jana wa viongozi wa mataifa ya Ulaya, kuhusu kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa fedha unaoendelea, baadhi ya serikali tayari zimeanza kutoa wazi mpango wake.

Uingereza mbali na kuwa haitumii sarafu ya Euro, lakini kama mwana chama wa Umoja wa Ulaya,imeanza kutekeleza kile serikali ya Gordon Brown inachoona kama kuunusuru mfumo wa fedha.

Uingereza imetoa dola billioni 64 kama dhamana ya kuzipiga jeki benki tatu mashuhuri nchini humo. Benki hizo ni HBOS,Lloyds TSB na Royal bank of Scotland RBS. Hatua ya kuipiga jeki benki ya RBS imepelekea Mkuu wa benki hiyo kujiuzulu.

Waziri wa fedha wa Uingereza, Alistair Darling, amesema kuwa wakati mgumu unasababisha kuchukua hatua ngumu na kuongeza kuwa yuko tayari kuongeza dau zaidi ikiwa litahitajika.

Na hapa Ujerumani viongozi wa serikali ya muungano,kimsingi wameunga mkono hatua muafaka za kuupiga jeki mfumo wa fedha wa Ujerumani.Katika mkutano wa jana nchini Ufaransa, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, alisema makubaliano ya viongozi wa kuimarisha uchumi yalikuwa na lengo la kuleta uwiano katika kanda ya Euro.

Katika hali inayoonekana kama kukubaliana na mpango huo hapa Ujerumani viongozi wanaounda serikali ya muungano,Kansela mwenyewe,makamu wake,Frank-Walter Steinmeier pamoja na waziri wa fedha Peer Steinbrück, watafanya kikao cha baraza la mawaziri baadae leo jumatatu ili kuelezea kinagaubaga mpango wenyewe.

Serikali ya Berlin haikuweza kutoa maelezo zaidi ya mpango huo lakini wachambuzi wanasema mpango wa kuunusuru mfumo wa fedha wa Ujerumani unaweza ukafikia Euro billioni 400.

Benki kuu ya Ulaya nayo imeingilia kati na kutangaza kuwa ikishirikiana na benki kuu zingine itatoa mabillioni ya dola kadhaa ambazo zitatumiwa na benki za kibiashara.

Mkuu wa benki kuu ya Ulaya, Jean-Claude Trichet akitangaza hatua hiyo za pamoja hata hivyo alisema kuwa taasisi yake imechukua hatua za kutosha.

Hatua za sasa za benki kuu ya Ulaya pamoja na za serikali mbalimbali zimepelekea kupanda kwa bei za hisa katika masoko mbalimbali katika bara la Ulaya.

Faharasa katika masoko ya hisa ya Ulaya baada ya kufunguliwa jumatatu zilipanda karibu asili mia tano.

Katika soko la hisa la hapa Ujerumani la mjini Frankfurt,hisa zilipanda wakati bishara zilipoanza leo jumatatu.Katika faharasa ya DAX-30 ilipanda kwa asili mia 5.4.

Hii inaonyesha kama wawekezaji wa Ujerumani wamepewa moyo na uamuzi wa viongozi wa Ulaya katika kikao chao cha jana.Na serikali ya Ujerumani baadae leo jumatatu inatarajiwa kutoa maelezo zaidi ya mpango wake wa kuupiga jeki mfumo wa fedha.