1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ghuba yawania kuimarisha ushirikiano

14 Desemba 2021

Wakuu wa mataifa ya Ghuba ya Kiarabu wamekutana hii leo kwa ajili ya mkutano wa kilele wa kila mwaka unaotarajiwa pamoja na masuala mengine kusisitiza mshikamano baina yao baada ya mgawanyiko mkubwa

https://p.dw.com/p/44Fkz
Katar | Ankunft Mohammed bin Salman in Doha
Picha: Bandar Aljaloud/Saudi Royal Palace via AP/picture alliance

Wakuu hawa wanasaka nia hiyo huku kukiwa na wasiwasi wa kikanda dhidi ya Iran pamoja na kuongezeka kwa mvutano wa kiuchumi ndani ya ukanda huo unaozalisha kiwango kikubwa cha mafuta ulimwenguni. 

Kabla ya mkutano huo wa kilele, mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman alizuru mataifa ya Ghuba, ikiwa ni karibia mwaka mmoja baada ya Riyadh kuumaliza mzozo wa kidiplomasia na Qatar. Kwenye ziara hiyo emir wa Qatar alisisitiza kwamba ziara hiyo itaimarisha mahusiano ya kihistoria hasa baada ya mzozo huo.

Soma Zaidi:Mkutano wa kilele wa mataifa ya Ghuba wafanyika Saudia 

Saudi Arabia na Misri ambayo si miongoni mwa mataifa hayo ya Ghuba wamerejesha mahusiano hayo ya kidiplomasia na Doha, lakini Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain bado hawajarejesha, ingawa Abu Dhabi iko katika mchakato wa kurejesha mahusiano hayo. Ikumbukwe kwamba Saudi Arabia,Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri zilikata mahusiano ya kidiplomasia kufuatia madai kwamba inaunga mkono ugaidi na ilikuwa na mahusiano ya karibu na mpinzani wako mkubwa Iran. Doha inakana madai hayo.

Saoudi Arabien Prinz Mohammed bin Salman Al Saud
Mwanamfalme mohammed bin Salman wa Saudi Arabia alizuru mataifa ya Ghuba kwa lengo la kuimarisha mahusiano miongoni mwaoPicha: BARNI Cristiano/ATP photo agency/picture alliance

Afisa mwandamizi kutoka Umoja wa Ufalme wa Kiarabu Anwar Gargash amekiri wiki iliyopita kwamba kuna maeneo yatahitaji muda, lakini akasema kiuhalisia, ushirikiano baina ya mataifa ya Ghuba unarejea kama awali.

Vyombo vya habari nchini Saudi Arabia vimesema ziara ya mwanamfalme Mohammed bin Salman ililenga kuangazia mshikamano wakati mataifa makubwa ulimwenguni yakisaka kuyafufua makubaliano ya nyuklia na Iran, katika wakati ambapo hali ya sintofahamu kuhusiana na jukumu la Marekani kwenye katika eneo la Ghuba pia ikiongezeka.

Waislamu wa madehebu ya Sunni wa Saudi Arabia na Washia wa Iran kwa pamoja wanawania kuwa na ushawishi katikati ya mivutano kwenye ukanda huo ambayo ilichochewa pamoja na masuala mengine vita vya Yemen na Lebanon ambako ushawishi wa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran unaozidi kuimarika umevuruga mahusiano kati ya Beirut na na mataifa hayo.

Rais mpya wa Iran na mwenye msimamo mkali Ebrahim Raisi tayari amekwishasema kwamba kipaumbele cha sera yake ya nje kitakuwa ni kuimarisha mahusiano na majirani zake wa Ghuba.

Katibu mkuu wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba- GCC Nayef Al-Hajraf alikiambia kituo cha televisheni cha Saudi Arabia kabla ya mkutano huo wa kilele kwamba Iran inatakiwa kuonyesha ishara ya nia njema. Abu Dhabi iliimarisha mahusiano yake na Iran na Uturuki kwa haraka zaidi baada ya kurejesha mahusiano yake na Israel.

Mashirika: RTRE