1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya G20 na hatma ya Afrika

6 Julai 2017

Wakati Ujerumani ikiwapokea wakuu wa nchi za G-20, Kansela Angela Merkel anayo haki ya kujisikia kama kiongozi wa nchi hizo akiipokonya uongozi Marekani inayoonekana kama imepoteza mwelekeo chini ya utawala wa Trump

https://p.dw.com/p/2g3sH
G20 Gipfel in Hamburg | Logo
Eneo ambalo mkutano wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda utafanyika mjini HamburgPicha: picture-alliance/Sputnik/A. Pantcykov

Swali ni iwapo Merkel anaweza kuwa na muda wa kushughulikia matatizo ya kiuchumi yasiyokwisha ya bara la Afrika, anasema Jenerali Ulimwengu katika maoni yake.

Tansania Jenerali Ulimwengu Journalist
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Jenerali UlimwenguPicha: privat

Klabu hiyo ya nchi matajiri inaanza mkutano wake wikendi hii katika jiji la pwani ya kaskazini, Hamburg, huku nchi hizo zikiwa zinakabiliwa na agenda za matatizo mazito kama vile ugaidi na usalama, wimbi la wahamiaji, mabadiliko ya tabia-nchi, jeuri ya Korea ya Kaskazini juu ya mpango wake wa silaha za nyuklia na uwezekano wa mapambano ya wanaharakati wanaopinga utandawazi na ubepari.

Inawezekana vipi kutaraji kwamba wakuu wa serikali ya Ujerumani, pamoja na nchi nyingine za G-20, wataweza  kupata wasaa wa kushughulikia matatizo ya Afrika yaliyoshindikana kwa muda mrefu ingawa bara hili limejaribu mikakati kadhaa isiyofanikiwa huku likishindwa kutumia utajiri mkubwa wa nchi zetu?

Hata hivyo, inavyoelekea hivyo ndivyo wakuu wa Ujerumani walivyodhamiria kufanya, Mkutano wa Hamburg umetenga nafasi na muda wa kutosha kwa ajili ya ajenda wanayoiita "Mkataba na Afrika” (Compact with Africa), ambao serikali ya Ujerumani imeueleza kama mkakati wa "kupanga jinsi ya kuandaa mpango wa kiuchumi unaoaminika utakaoongeza fursa za uwekezaji, utakaoimarisha miundombinu na utakaotengeneza ajira zaidi miongoni mwa nchi za Afrika ili kuchangia kufanikisha Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.”

Ushawishi wa Ujerumani duniani

G20 Gipfel Bundestag Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/J.MacDougall

Ujerumani ilichukua uongozi wa G-20 Desemba 2016, na imekusudia kutumia ushawishi wake unaoongezeka duniani kujaribu kuleta mabadiliko barani Afrika. Mkutano wa Hamburg unaonekana kama jukwaa muhimu kwa ajili ya uzinduzi wa mkakati huu mpya wa Merkel.

Waandaji wa mkutano wa Hamburg wanatumai kuwa na maelewano baina ya maofisa wa Ujerumani na wawakilishi wa chi za Kiafrika walioko Hamburg kwa ajili ya mkutano huo. Mwezi Juni wakuu kadhaa wa nchi za Afrika walikutana na wenzao wa Ujerumani mjini Berlin  na kukubaliana juu ya maeneo waliyoamua kuyapa kipaumbele, ambayo ni ajira vijijini, maendeleo ya rasilimali-watu, kilimo, elimu ya teknolojia kwa mabinti, maendeleo ya viwanda, amani na usalama, na mapambano dhidi ya ufisadi.

Baadhi ya wanaharakati nchini Ujerumani wamekuwa wakizungumzia "Marshall Plan” kwa ajili ya Afrika, hii ikikumbushia mpango kabambe wa Marekani kufufua uchumi wa nchi za Ulaya baada ya uharibifu mkubwa wa Vita Kuu ya Pili. Wako wanaouita mpango huu "Mpango wa Merkel.”

Hata hivyo, kuulinganisha mpango wa Ujerumani na "Marshall Plan” ni kukoleza mno chumvi kwa sababu hali ya Ulaya iliyoifanya Marekani iingie kwa nguvu kubwa kunusuru uchumi wa nchi za Ulaya ni tofauti na hali iliyomo barani Afrika na uhusiano baina ya bara hili na nchi za Ulaya.

Kuchoka kwa wafadhili

Kwanza kabisa, Vita Kuu ya Pili ilihusu iliwahusu Wazungu, na Marekani iliingilia katika vita hiyo na ufufuaji wa uchumi baada ya vita ili kuwanusuru "ndugu” zake, na hiyo siyo hali tuliyo nayo hapa. Aidha, kuna mtazamo kwamba misaada mingi ya kifedha na kiuchumi inayotolewa kwa nchi za Afrika huishia kutumbukia katika lindi lisilo na kikomo, ambalo limesababisha "mchoko wa wafadhili.”

Masuala ya ufisadi na utamaduni wa utawala mbovu yanalifanya bara la Afrika lionekane kama la hovyo machoni mwa wachambuzi wa magharibi, ambao hawaoni sababu ya kuendelea kutoa misaada kwa nchi za Afrika. Pia, imeelezwa kwamba Afrika imeshindwa kutekeleza mipango yake iliyojipangia, kama "Lagos Plan of Action” wa mwaka 1980 na NEPAD.

Mipango iliyobuniwa nje ya bara la Afrika, kama vile "Kamisheni ya Blair” ya miaka ya 1990, haikufua dafu na haionyeshi kwamba mipango mipya inayobuniwa ughaibuni itazaa matunda yo yote chanya.

Hata hivyo, Kansela Merkel amejidhihirisha kuwa "mwanamke wa shoka” kwa matendo yake katika nyanja nyingine. Mafanikio yake katika utekelezaji wa mpango wake kabambe wa Willkommenkultur kuhusu wakimbizi wa Mashariki ya Kati umedhihirisha ukakamavu wake; na waziri wake wa ushirikiano wa maendeleo, Gerd Muller, ametamka waziwazi wasiwasi wake iwapo hatua madhuhubuti hazitachukuliwa kupambana na ufukara uliokithiri barani Afrika, kwa kusema kwamba inawezekana kuwaona wakimbizi milioni miloni 100 wa kiuchumi  wakibisha hodi mlangoni mwa Ujerumani. Wazo  kamahilo linaweza kuwatia shime Wajerumani kuchukua hatua kama hizi tunazoshuhudia.