1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya EU yaonywa

MjahidA16 Aprili 2013

Umoja wa Ulaya umezionya nchi wanachama wa Umoja huo kuweka mikakati imara dhidi ya biashara ya kuuza binaadamu isiokubalika au ziwekewe vikwazo.

https://p.dw.com/p/18GeL
Bendera za mataifa ya Umoja wa Ulaya
Bendera za mataifa ya Umoja wa UlayaPicha: Getty Images/AFP

Ripoti ya halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, imesema tangu mwaka wa 2008 hadi mwaka wa 2010 biashara ya kuuza watu imeongezeka kwa asilimia 18 katika mataifa 27 yanayounda Umoja wa Ulaya.

Kulingana na kamishna anayeshughulika na maswala ya jamii katika Umoja huo Cecilia Malmstroem, Wanawake wanaume na watoto wanaendelea kuuzwa katika biashara ya ngono, kazi ngumu, ndoa za kulazimishwa, kazi za nyumbani, kuomba au hata kutolewa sehemu zao za mwili kwa ajili ya biashara. "Huu ni ukweli unaouma," alisema kamishna Malmstroem.

Utafiti uliofanywa mwezi Juni mwaka jana na shirika la kazi duniani, ulikadiria takriban watu 880,000 walilazimika kufanya kazi ngumu katika mataifa ya Ulaya, jambo ambalo linatarajiwa kuongezeka kutokana na mgogoro wa uchumi, unaoshuhudiwa kwa sasa katika baadahi ya nchi, kwasababu raia katika nchi hizo hutafuta ajira za aina yoyote ile ili waweze kujikimu kimaisha.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya katika maswala ya Jamii Cecilia Malmstroem
Kamishna wa Umoja wa Ulaya katika maswala ya Jamii Cecilia MalmstroemPicha: AP

Ripoti hiyo iliotolewa jana imeonesha watu 7 kati ya kumi wanaouzwa ni wanawake, asilimia 17 ya wanaume, asilimia 12 ya wasichana huku asilimia 3 ikiwa ni ya watoto wadogo wa kiume. zaidi ya nusu ya waathiriwa yani asilimia 61 wanatokea katika mataifa ya Umoja wa Ulaya hasa Romania na Bulgaria wakati Nigeria na China ni katika mataifa yanayojulikana sana kwa jambo hilo nje ya bara la ulaya.

Kamishna Cecilia Malmstroem amesema japo ripoti ilionesha kukamatwa kwa wanaoendesha biashara za kuuza watu, mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya yameshindwa kutekeleza mikakati thabiti dhidi ya biashara hiyo, mikakati ambayo ilikubalika mwaka uliopita.

Mataifa machache yatekeleza mkakati wa EU

Kati ya nchi 27 ni nchi 6 tu zilizotilia maanani mikakati hiyo iliowekwa na Umoja wa ulaya. Nchi kama Jamhuri ya Czech, Finland, Latvia, Hungary, Poland na Sweden ndizo zilizo tekeleza hatua hiyo huku Ubelgiji, Lithuania na Slovenia zikionekana kutaka kuchukua mwelekeo kama huo.

Sasa Umoja huo umetaka kila nchi kutilia manani kuweka sheria ya kudhibiti biashara hiyo au iwekewe vikwazo. Bara la Ulaya miaka miwili iliopita ilikubali kusimama kidete dhidi ya biashara hiyo inayokadiriwa kuingiza euro bilioni 2.5 kila mwaka kwa kupanua ufafanuzi juu ya uhalifu huo na kulenga masuala ya ngono, kazi ngumu, kuomba na kutolewa kwa sehemu za mwili na kuweka sheria kali za kuendana na hilo.

Wanafunzi Romania wakionesha athari za biashara ya kuuza watu
Wanafunzi Romania wakionesha athari za biashara ya kuuza watuPicha: AP

Mikakati hiyo mipya inajumuisha miaka mitano kwa atakayepatikana na makosa na miaka kumi kwa kosa lolote litakalojumuisha utumiaji wa watoto au mateso au uhalifu. Hatua nyengine ni kukubalika kwa mataifa hayo kuchukua uamuzi wa kimahakama nje ya nchi yake katika tukio ambalo limetendwa na raia wa nchi yake au mkaazi wa nchi hiyo.

Hata hivyo Utafiti uliofanywa na shirika la kazi duniani mwaka 2012, ulionesha watu milioni 21 duniani kote ni waathirika wa biashara hii ya kuuza watu isiokubalika.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman