Mataifa ya Bonde la Nile yakutana Dar es Salaam
22 Februari 2022Yakikutana kwa pamoja jijini Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya bonde la mto Nile, mataifa hayo yameonyesha namna yanavyopaswa kuendelea kushirikiana hasa wakati ambapo maji yanaendelea kuwa rasilimali muhimu inayobeba dhamana yote ya maisha ya viumbe hai.
Bonde la mto Nile ambao chanzo chake ni ziwa Victoria kwa miaka kadhaa lilikuwa kiini cha mivutano miongoni mwa nchi zilizopitiwa nalo, lakini kuwepo kwa ushirikiano wa mpito ulioasisiwa jijini Dar es Salaam mnamo mwaka 1999 kumesaidia kuzika mivutano hiyo.
Katibu mkuu wizara ya maji nchini Tanzania, Mhandisi Anthony Sanga anasema mikutano ya mara kwa mara inayozileta pamoja nchi husika, imesaidia kufanya matumizi ya maji ya mto huo kuwa endelevu.
Mkutano huo wa Dar es salaam ambao ni sehemu ya maadhimiisho ya siku ya bonde la mto Nile umewaleta pamoja mawaziri wanaohusika na sekta ya maji, mazingira, wataalamu wa mazingira na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa.
Makamu wa rais wa Tanzania, Dr Philip Mpango aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alihimiza namna mataifa yanayofaidika na mto huo yanavyopaswa kuwa wasikivu kulinda mazingira yake ili kulinda uhai wake.
Baadhi ya nchi zinazopitiwa na bonde la mto Nile ni pamoja na Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Sudan, Misri, Burundi, Rwanda pamoja na Sudan Kusini.
Mto Nile wenye urefu wa kilometa 6,695 ni mto mrefu zaidi duniani huku ukitegemewa na mataifa mengi wakati nchi kama Misri ikitajwa ndiyo inayotumia kiasi kikubwa zaidi cha maji yake kwa shughuli za kilimo na mahitaji mengine.
George Njogopa, DW, Dar es Salaam