Mataifa kadhaa ya Asia yakumbwa na mvua kubwa
5 Julai 2023Mataifa kadhaa barani Asia yanashuhudia mvua kubwa za msimu ambazo tayari zimesababisha vifo vya makumi ya watu na kuwalazimisha mamia wengine kuyakimbia makaazi yao.
Vyombo vya habari vya China vimeripoti kuwa watu 15 wamepoteza maisha na wengine 4 hawajulikani waliko baada ya mvua kunyesha kwenye upande wa kaskazini magharibi. Mvua hizo za tangu siku ya Jumatatu zimeleta maafa makubwa kwenye mji Chongqing na mkoa wa Sichuan.
Soma pia: Mafuriko yaitikisa China
Nchini Pakistan watu 18 wamekufa, barabara zimesombwa na maji na makaazi yameharibiwa kutokana na mvua zinazoendelea. Miji ya Lahore kwenye mkoa wa Punjab na mji mkuu Islamabad ndiyo imeshuhudia kiwango cha mvua kinachovunja rikodi. Kwenye taifa jingine la Mongolia, mamia ya watu kwenye mji mkuu Ulaanbaatar wamezikimbia nyumba zao kufuatia mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.