1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa 90 yalaani Israel kuwaadhibu Wapalestina

18 Januari 2023

Katika hatua nadra sana kuchukuliwa panapohusika mzozo wa Mashariki ya Kati, zaidi ya mataifa 90 duniani yametoa tamko la pamoja kulaani vikwazo vya Israel dhidi ya Wapalestina na kutaka visitishwe mara moja.

https://p.dw.com/p/4MLz8
Kabinettssitzung in Israel
Picha: Atef Safadi/Pool European Pressphoto Agency/AP/dpa/picture alliance

"Kuhusiana na suala hili, tunasikitishwa sana na uamuzi wa serikali ya Israel kutekeleza vitendo vinavyolenga kuwaumiza kwa makusudi watu wa Palestina, uongozi wao na asasi za kijamii, kufuatia ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  kutaka maoni ya kitaalamu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki." Inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyochapishwa siku ya Jumanne (Januari 17).

Miongoni mwa mataifa yaliyosaini waraka huo wa kimataifa unaotaka pia kusitishwa mara moja kwa hatua hizo za Israel, ni pamoja Ujerumani, Ufaransa, Italia na Brazil.

Soma zaidi: Israel kuchukua hatua baada ya Palestina kwenda ICJ

Hatua hizo za kuwaadhibu Wapalestina zilitokana na azimio la Umoja wa Mataifa kutaka lipate ushauri kutoka Mahakama hiyo kuu ya kimataifa juu ya ukaliaji kimabavu wa Israel kwenye maeneo ya Wapalestina.

Hata hivyo, Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa, Gilad Erdan, aliliita tamko hilo kuwa "halina maana yoyote".

"Kila nchi ambayo imesaini tamko hilo imeumwagia mafuta moto wa uchochezi na ugaidi wa Palestina na imeharibu fursa yoyote ile ya muafaka." Alisema balozi huyo wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha Channel 12.

Soma zaidi: Baraza la Usalama lakutana kuhusu mzozo wa Palestina

Mwishoni mwa mwezi Disemba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura ya kufanyika mapitio ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki mjini The Hague juu ya ukaliaji huo ulioanza mwaka 1967. 

Israel yalipiza kisasi

Katika kulipiza kisasi kwa uamuzi huo, Israel iliamua kupitisha hatua kadhaa za kuwaadhibu Wapalestina ikiwemo kutwaa dola milioni 40 za kodi ya mapato zilizokusanywa na Israel kwa ajili ya serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kuzilipa familia za Waisraeli waliopoteza maisha yao kwenye mashambulizi yaliyofanywa na Wapalestina.

Jerusalem Tempelberg
Sehemu ya Mji Mkongwe wa Jerusalem Mashariki ambao Wapalestina wanataka uwe mji mkuu wa taifa lao huru.Picha: Moritz Wolf/imagebroker/IMAGO

Vile vile, serikali ya Israel ilisema inapanga kuyachukulia hatua mashirika iliyodai yanashajiisha 'harakatik za kigaidi" kwa jina la kazi za kibinaadamu. 

Soma zaidi: Nchi za kiarabu zaahidi kuendelea kuiunga mkono Palestina

Tayari Waziri Mkuu wa Palestina, Mohammad Shtayeh, ameshaonya juu ya uwezekano wa kuporomoka kwa serikali yake. 

Israel iliuteka Ukanda wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, miongoni mwa maeneo mengine, mwaka 1967. 

Hivi leo, zaidi ya walowezi 600,000 wa Kiisraeili wanaishi kwenye maeneo hayo, ambayo Wapalestina wanayadai kuwa sehemu ya dola lao huru na upande wa Jerusalem Mashariki kuwa mji wao mkuu. 

Israel kwa upande wake, haioni kuwa sera yake ya makaazi ya walowezi inakwenda kinyume na sheria za kimataifa.

Chanzo: dpa