Masuala muhimu yafikiwa na Viongozi wa nchi za G7
9 Juni 2015Rais Obama amesema baada ya mkutano na viongozi wenzake katika mkutano wa G7 kuwa kuna haja ya dharura ya kutafuta njia ya kuitatua hali ya kiuchumi Ugiriki lakini suluhisho hilo linaihitaji Ugiriki kuonyesha ukakamavu katika kufanya mageuzi muhimu sio tu ya kuwaridhisha wakopeshaji wake lakini pia kuanza kujenga msingi wa kuukuza uchumi wa nchi hiyo na kustawi kwa mara nyingine.
Obama pia amewataka wakopeshaji wa Ugiriki kulegeza msimamo wao ili mgogoro huo wa kiuchumi uweze kupatiwa ufumbuzi. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameitaka Ugiriki kuyapa kasi mazungumzo kuhusu mageuzi ya kiuchumi ili nchi hiyo iweze kupata mkopo.
Kwa upande wake Rais wa Ufaransa Francois Hollande pia amesisitiza muda wa mwisho kwa Ugiriki na wakopeshaji kufikia makubaliano unapaswa kuwa mwezi huu wa Juni.
Ugaidi, biashara na mazingira yaangaziwa
Mbali na kutuama zaidi kuhusu kitisho cha makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali nchini Syria, Iraq na makundi ya waasi kama ya Boko Haram barani Afrika, kulaani ubabe wa Urusi katika mzozo wa Ukraine na namna za kuboresha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo, viongozi hao kutoka Ujerumani, Marekani, Ufaransa, Japan, Canada, Italia na Uingereza wamekubaliana kupunguza viwango vya joto duniani hadi nyuzi mbili kwa kuweka mikakati ya kupunguza gesi chafu ya Carbon inayotoka viwandani.
Tangazo hilo limeongeza matumaini ya kufikiwa makubaliano muhimu kuhusu mazingira yanayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa baadaye mwaka huu mjini Paris Ufaransa. Merkel amesifiwa kwa kuongoza kampeini ya kuwashawishi viongozi wake kufikia makubaliano hayo muhimu ya mazingira na ametajwa 'kansela wa mazingira'.
Viongozi hao wa nchi zilizostawi zaidi kiviwanda duniani pia wameahidi kulitokomeza janga la Ebola kwa kutoa msaada kwa takriban nchi sitini zikiwemo za magharibi mwa Afrika katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuepusha kuzuka kwa miripuko ya magonjwa.
Majanga ya afya kushughulikiwa haraka
Nchi hizo za G7 zimesema zitashirikiana kupambana na majanga ya kiafya katika siku za usoni na kuweka mikakati haraka ikiwemo kuwatuma wataalamu haraka iwezekanavyo kudhibiti hali.
Hata hivyo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamevunjwa moyo na tamko hilo kwani halijafafanua wazi ni hatua zipi madhubuti zitachukuliwa kushughhulikia na kuzuia majanga kama ya Ebola.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la madaktari wasio na mipaka MSF nchini Ujerumani Florian Westphal amesema vingozi hao hawajafanya mengi kuhakikisha majanga ya kiafya hayatasambaa kupita viwango vya kudhibitiwa ipasavyo katika siku za usoni. Shirika la Oxfam pia limeelezea kutoridhishwa na hatua dhaifu zilizochukuliwa na viongozi hao wa G7.
Viongozi hao waliohitimisha mkutano wa siku mbili hapo jana mjini Elmau, nchini Ujerumani pia wamesema watatenga fedha za kuzuia na kudhibiti magonjwa yaliyotelekezwa yanayoathiri maeneo ya joto ili kutimiza lengo la kuyatokomeza magonjwa hayo ifikapo mwaka 2020.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/ap/Afp
Mhariri: Yusuf Saumu