Masoko yapanda leo baada ya mataifa kadha kuahidi kutoa fedha.
14 Oktoba 2008Masoko ya hisa yamepanda kwa siku ya pili mfululizo leo Jumanne, huku soko la mjini Tokyo likionyesha kupanda kwa kiwango cha juu kabisa baada ya serikali kadha duniani kote kutoa mwelekeo wa kuzinusuru benki zenye matatizo kutokana na mzozo mkubwa kabisa wa kifedha uliopo hivi sasa. Marekani itatangaza hii leo mpango wa kuingiza kiasi cha Dola bilioni 250 katika mabenki yake ikiwa ni hatua muhimu katika kuupatia mfumbuzi mzozo huu wa kifedha duniani , kufuatia mataifa ya Ulaya kufanya hivyo.
Soko la hisa mjini Tokyo lilifungwa likiwa limefikia kiwango cha asilimia 14.15 wakati Japan ikitangaza hatua za kuimarisha masoko ikiwa ni pamoja na ulegezaji wa vikwazo dhidi ya ununuzi wa hisa za makampuni kwa makampuni.
Katika mataifa ya Ulaya , soko la hisa la mjini London lilipanda kwa asilimia 3.40 katika mauzo ya mapema leo.
Jana Jumatatu soko hilo lilifungwa likiwa limepanda kwa kiwango cha asilimia nane , wakati Uingereza ikimimina mabilioni ya dola katika masoko yenye upungufu mkubwa wa fedha za kukopa na kununua hisa katika baadhi ya mabenki makubwa ya biashara nchini humo.
Ni mapema mno kusema iwapo mwelekeo halisi wa uaminifu na imani imerejea katika masoko, lakini inaonyesha kana kwamba tumekaribia, amesema mkuu wa taasisi moja ya fedha Martin Slaney.
Na ameongeza kuwa siku nyingine ya kihistoria kwa soko la hisa la Wall Street inaonyesha wimbi la uhai ambalo unaweza kulihisi katika masoko kutokana na hatua za kunusuru masoko.
Masoko ya Marekani yamepanda kwa zaidi ya asilimia 11 jana Jumatatu, na kulinyanyua soko la Dow Jones kwa kiwango ambacho hakijawahi kuonekana kwa muda wa miaka 75, wakati serikali ya Marekani mjini Washington ikisema kuwa itanunua hisa katika makampuni kadha.
Rais wa Marekani George W. Bush na waziri wa fedha Henry Paulson wanatarajiwa kutoa taarifa zao leo Jumanne kuhusu hatua hiyo inayochukuliwa na serikali pamoja na serikali kadha nyingine duniani. Akizungumzia mpango wa mataifa ya Ulaya wa uokozi rais Nicolas Sarkozy ametoa uhakikisho kwa mabenki na masoko ya fedha kuwa yatapata fedha kwa ajili ya shughuli zao bila matatizo.
Katika mauzo ya asubuhi ya leo, soko la hisa la mjini Paris lilipanda kwa asilimia 4.18, siku moja baada ya kupanda kwa kiwango cha asilimia 11, ikiwa ni kiwango chake cha juu kabisa kupanda kwa siku moja.
Viongozi wa mataifa ya Ulaya jana Jumatatu walifungua njia kwa ajili ya kutolewa kiasi cha Euro trilioni moja katika mpango wa uokozi kwa ajili ya sekta ya benki yenye matatizo, wakiahidi kuingiza mitaji katika benki ambazo zimeathirika zaidi na ambazo zimelazimika kufuta madeni makubwa ambayo hayalipiki baina ya wadau wa mambo ya fedha.
►◄