1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masoko ya hisa na fedha yaanza kuyumba

15 Aprili 2020

Baada ya ubashiri wa IMF kuwa uchumi wa ulimwengu utakabiliwa na anguko kubwa kabisa tangu lile la miaka 1930 kutokana na athari za kirusi cha corona, hisa kwenye masoko kadhaa ya fedha ulimwenguni zimeanza kuporomoka.

https://p.dw.com/p/3awpd
Gita Gopinath IMF Chef-Ökonomin
Picha: Imago Images/Xinhua/Liu Jie

Masoko kwenye miji ya Tokyo na Hong Kong yalisalia kama yalivyokuwa kabla ya tangazo hilo lakini masoko ya hisa ya Shanghai na Sydney yaliporomoka licha ya usiku wake kutanguliwa na ongezeko kwenye soko la Wall Street kufuatia mauzo makubwa kwenye hisa za teknolojia.

Utabiri wa hivi karibuni kabisa wa Shirika hilo la fedha la kimataifa ulionesha kwamba uchumi utayumba kwa asilimia 3 mwaka huu, likiwa ni anguko kubwa kuliko la mwaka 2009, ambapo uchumi ulishuka kwa asilimia 0.1.

Shirika la IMF limetabiri kuwa uchumi utayumba kwa asilimia 3 mwaka huu.
Shirika la IMF limetabiri kuwa uchumi utayumba kwa asilimia 3 mwaka huu.Picha: AFP/K. Nogi

Utabiri huu ni kinyume kabisa na ule wa mwezi Januari ambapo IMF ilitabiri kuwa uchumi wa dunia ungelipanda kwa asilimia 3.3, ingawa hapo ilikuwa ni kabla ya mripuko wa kirusi cha corona haujazilazimisha serikali ulimwenguni kufunga viwanda, safari za ndege na sekta nyengine za kuzalisha mali, bidhaa na huduma kote duniani.

Kwa sasa wawekezaji kwenye hisa za masoko wanatupia macho yao kwenye jinsi gani na lini serikali zitaanza kulegeza masharti ya zuio la shughuli za kibiashara na mienendo ya watu yaliyowekwa ili kuzuwia kasi ya kusambaa kwa kirusi cha corona.

Wachambuzi wa masuala ya fedha na uchumi wanasema dunia itapoteza pato la jumla la takribani dola trilioni 9, ambayo ni zaidi ya chumbi kubwa za Ujerumani na Japan zikichanganywa pamoja.

Wachambuzi wasema dunia itapoteza pato la jumla la takribani dola trilioni 9.
Wachambuzi wasema dunia itapoteza pato la jumla la takribani dola trilioni 9.Picha: picture-alliance/dpa/M. Nagle

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akijadiliana na maafisa wake juu ya namna ya kuondosha marufuku zilizowekwa, huku magavana wa majimbo kadhaa ya nchi hiyo nao wakifikiria kuanza kuzifunguwa kidogo kidogo chumi za majimbo yao, lakini katika namna ambayo hawatachochea kurejesha upya kasi ya maambukizi mapya.

Katika mataifa ya Italia, Uhispania na maeneo kadhaa barani Ulaya ambako kasi ya maambukizi mapya na vifo imeanza kushuka, mchakato wa kuzifungua chumi zao umeanza. Tayari baadhi ya maduka na viwanda vimeruhusiwa kuanza tena kazi katika jitihada na kuoanisha maslahi ya kiafya na yale ya kiuchumi.