1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masoko ya fedha yashusha pumzi

Saumu Ramadhani Yusuf2 Januari 2013

Masoko ya fedha yameimarika kote duniani kufuatia hatua ya makubaliano ya bajeti nchini Marekani na kuepusha ongezeko la kodi kwa wananchi. Wadadisi wa masuala ya kiuchumi wanasema balaa kubwa limeepukwa.

https://p.dw.com/p/17CYf
Mteja akifuatilia Soko la hisa la Frankfurt Ujerumani
Mteja akifuatilia Soko la hisa la Frankfurt UjerumaniPicha: REUTERS

Wadadisi wa masuala ya kiuchumi wanasema makubaliano hayo ya bunge la Marekani yameepusha kizingiti kikubwa cha kiuchumi kilichokuwa kinawakabili wawekezaji. Hata hivyo wanaonya kwamba bado hatari ipo katika masoko ya fedha kwa kuwa wasiwasi wa kisiasa utaendelea kuwepo katika miezi kadhaa ijayo.

Baada ya wabunge wa Marekani kukubaliana juu ya Muswaada wa rais Barack Obama wa kutaka mfumo wa utozaji kodi unaowapendelea matajiri ubadilishwe, masoko ya fedha duniani kote yameonekana kuimarika ambapo hapa barani Ulaya faharasa za soko la hisa la Benchmark Stoxx zilipanda kwa asilimia 1.9 huku hisa katika masoko ya barani Asia yakiripotiwa kuimarika pia.

Soko la Hisa la Japan
Soko la Hisa la JapanPicha: AP

Wasiwasi waondoka

Wadadisi wa masuala ya kiuchumi wanasema hatua ya wajumbe wa baraza la wawakilishi linalodhibitiwa na chama cha Republicans nchini Marekani ya kuunga mkono muswaada huo ambao umeungwa mkono pia na baraza la seneti imeepusha balaa kubwa la kiuchumi pamoja na kuwaondolea mashaka wawekezaji duniani.

Hata hivyo wadadisi hao pia wanaonya kwamba pamoja na kitisho kikubwa zaidi cha kulemaza ukuaji wa uchumi duniani kimeondoka bado wasiwasi wa kisisasa utaendelea kuwepo katika miezi inayokuja.Mwanauchumi wa benki ya biashara ya Ujerumani ya Commerzbank Christoph Balz anasema makubaliano yaliyofikiwa na wabunge nchini Marekani hayatotatua changamoto za kimsingi kama vile mageuzi ya mfumo wa kodi na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kijamii.

Hata hivyo masoko ya makubwa ya hisa hasa barani Ulaya yameshusha pumzi kwa kiasi kikubwa huku yakionekana kupata motisha zaidi yaliyokuwa yameupoteza wakati majadiliano yalipokuwa yakiendelea mjini Washington hadi mwishoni mwa mwaka 2012.Hisa za Soko kubwa kabisa la hisa barani Ulaya,la London nchini Uingereza zimepanda kwa zaidi ya asilimia 2 na kupindukia alama ya 6000 kwa mara ya kwanza kabisa tangu Julai mwaka 2011.

Sarafu ya Yuro yapanda thamani dhidi ya Dola ya Marekani
Sarafu ya Yuro yapanda thamani dhidi ya Dola ya MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Afueni ya masoko ya Hisa

Hisa katika masoko ya Frankfurt na Paris pia zilipanda kwa zaidi ya 2 asilimia katika kipindi cha kwanza cha biashara katika mwaka mpya na kuonekana kuwa ni mwanzo mzuri.Nchini Marekani kwenyewe mambo sio mabaya ambapo soko la hisa la Wall Street limefungua kwa hisa zake kupanda kwa asilimia 1.6 hii leo.

Matumaini ya faraja kwamba uchumi wa Marekani sasa utabakia katika kiwango kizuri cha ukuaji yamesababisha kupanda kwa bei ya mafuta kwa 1.2 asilimia ambapo sasa lita moja inauzwa kwa dolla 92.95. Sambamba na hayo thamani ya sarafu ya Yuro imepanda kwa 0.5 asilimia dhidi ya Dolla kufikia leo asubuhi.Faraja hiyo imeleta matumaini hadi kwenye masoko ya hisa ya Japan na China ambako wasiwasi ulikuwa umetawala.

Mwandishi:Saumu Yusuf

Mhariri:Josephat Charo