Mashtaka mapya dhidi ya walinzi wa Blackwater
18 Oktoba 2013Waendesha mashtaka wanasema raia 14 ambao hawakuwa na silaha waliuwawa kwenye mauaji hayo, ambapo walinzi waliwamiminia risasi Wairaki. Mauaji hayo yalisababisha msuguano katika uhusiano kati ya Marekani na Irak na kuongeza wasiwasi juu ya hatu ya Marekani kutumia walinzi wa kampuni binafsi za usalama, ambao walikuwa na kinga dhidi ya kushtakiwa nchini Iraq.
Mashtaka ya kwanza ya Marekani yaliyowasilishwa dhidi ya walinzi wa kampuni ya Blackwater mnamo mwaka 2008, yalitupiliwa mbali mwezi Desemba mwaka 2009, yapata mwezi mmoja kabla tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo. Jaji wa mahakama moja ya Marekani alipitisha kwamba waendesha mashtaka walitakiwa kufanya mengi zaidi kuacha nje kauli walizozitoa walinzi hao wakiwa chini ya kitisho cha kupoteza ajira zao.
Kesi hiyo ilianzishwa tena mwaka 2011 na waendesha mashtaka wakaanza tathmini ndefu ya mashtaka ambayo wangeweza kuyathibitisha mahakamani. Kesi hii mpya inajumuisha mashtaka 33, yakiwemo mauaji bila kukusudia, jaribio la kuua bila kukusudia na kutumia silaha katika uhalifu wa kutumia nguvu. Walinzi wamesema hawana hatia kwa mashtaka hayo yanayofanana na yale yaliyowasilishwa dhidi yao miaka mitano iliyopita.
Majina ya walinzi hao ni - Paul Slough mwenye umri wa miaka 34, Nicholas Slatten; 29, Evan Liberty, 31; na Dustin Heard, 32. "Tumevunjika moyo kwamba wizara ya sheria imeamua kuendelea na kesi hii, ambayo tunaamini haina msingi wowote kabisa," amesema Dave Schertler, wakili wa Heard, katika taarifa yake.
Ni mauaji yasiyo halali
Waendesha mashtaka wamesema wanaume hao walitumia bunduki za kulenga shabaha, bunduki za rashasha na maguruneti wakati wa shambulizi la ufyetuliaji risasi katika uwanja wa Nisur mjini Baghdad, ambapo watu 14 waliuwawa na wengine 18 kujeruhiwa.
"Wakala nyingi za Marekani zilizohudumu nchini Iraq zilifanya hivyo kwa heshima na taadhima, lakini kama inavyotuhumiwa leo, watetezi hawa walitumia vibaya mamlaka yao kupitia shambulizi la kiholela dhidi ya raia ambao hawakuwa na silaha, shambulizi ambalo lilipitiliza uwezekano wa kuhalishwa," amesema wakili wa Marekani, Ron Machen, ambaye ni mwendesha mashtaka mkuu mjini Washington, katika taarifa yake.
Kumepangwa kufanyika kikao maalumu cha mahakama kuhusu kesi hiyo inayowakabili walinzi hao wa kampuni ya Blackwater Ijumaa wiki ijayo. Tarehe ya kusikilizwa kesi hiyo haijawekwa na wakili wao alisema kwenye kikao cha mwezi uliopita kwamba huenda ikachukua miaka kadhaa kabla kesi hiyo kuanza.
Mwezi uliopita waendesha mashtaka walifutilia mbali mashtaka dhidi ya mlinzi wa tano wa kampuni hiyo, Donald Ball, wakisema wametumia mamlaka waliyo nayo kuzingatia tathmini ya ushahidi uliopo dhidi yake. Kampuni hiyo ya Blackwater ilibadili jina na sasa inajulikana kama Academi na makao yake yako McLean katika jimbo la Virginia.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE
Mhariri: Saumu Yusuf