Mashitaka dhidi ya Habre yanaandaliwa
22 Julai 2012Wataalamu wa Umoja wa Afrika na maafisa wa Senegal wanatafuta namna ya kuandaa mashitaka dhidi ya dikteta wa zamani wa Chad Hissene Habre kwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binaadamu.
Siki chache zilizopita, Mahakama ya Haki ya Kimataifa, ICJ, iliamuru kuwa Habre mwenye umri wa miaka 70 lazima afunguliwe mashitaka au apelekwe Ubelgiji na Senegal ilikubali kumfungulia mashitaka mwaka huu. Habre anaishi kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Dakar.
Ametumia zaidi ya miaka 20 akiwa huru nchini humo kutokana na kizungumkuti cha nani amfungulie mashitaka kwa vitendo hivyo vya uhalifu dhidi ya binaadamu alivyovifanya wakati wa uatawala wake miaka ya 1982 hadi 1990.
Utawala wake ulikuwa wa ukandamizaji na uliyawinda makundi ya kikabila. Mwaka 1992 ripoti ya kamisheni ya ukweli iliarifu kwamba alihusika na mauwaji ya watu zaidi ya 40,000 kwa sababu za kisiasa pamoja na kuwatesa maelfu ya watu.
Senegal yakubali kumburuta mahakamani
Senegal imeahidi hapo siku ya Ijumaa (tarehe 20 mwezi Julai) kumpeleka mahakamani kiongozi huyo, baada ya mahakama ya ICJ kuamua kuwa ni ifungue kesi kwenye mahakama zake za kuamini kama haitamkabidhi mikononi mwa Ubelgiji.
Uamuzi huo ni hatua mpya katika kampeni ya muda mrefu inayoendeshwa na watetezi wa haki za binadamu kwa lengo la kumfungulia mashtaka Hissene Habre.
Wataalamu wa mambo ya sheria wanasema suala la Habre ambalo limewasilishwa na Ubelgiji dhidi ya Senegal ambako Habre anaishi, linaweka msingi wa sheria ya kuziwajibisha nchi zinazotoa hifadhi kwa madikteta, kuwafungulia mashtaka au kuwarudisha katika nchi zao ambako walitenda uhalifu.
Shaka kwa watawala wengine kama yeye
Uamuzi huo utawatia tumbo joto watawala wa zamani, kama Zine al Abidine Ben Ali wa Tunisia, alietimuliwa kufuatia harakati za mapinduzi katika nchi za kiarabu.Ben Ali sasa anaishi katika hifadhi ya kisiasa nchini Saudi Arabia. Serikali ya Habre inadaiwa kuwatesa na kuwaua wapinzani.
Kutokana na Ubelgiji kufanikiwa, nchi nyingine zitaweza kuziwajibisha nchi zinazotoa hifadhi ya kisiasa kuwafungulia mashtaka madikteta au viongozi wahalifu, kwa jumla.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na Ubelgiji dhidi ya Senegal inaonyesha ukakamavu wa wanaharakati wa haki za binadamu katika kutafuta njia mpya za kuwafikisha mahakamani viongozi wanaotenda uhalifu mkubwa, hata ikiwa wanajaribu kuwa mbali na sheria.
Mahakama ya kimataifa ya Haki ya mjini tha Hague imesema Senegal lazima imfungulie mashtaka ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu Hissene Habre. Katika hukumu yake mahakama hiyo imeeleza kwamba imebainika kwa kauli moja kuwa Jamhuri ya Senegal inapaswa, bila ya kuchelewa zaidi, kumfikisha Habre mbele ya idara zenye mamlaka, kwa lengo la kumfungulia mashtaka, ikiwa Senegal haitamrudisha nchini Chad.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na tume ya Chad, utawala wa miaka minane wa Hissene Habre ulihusika na vifo vya watu zaidi alfu 40 miongoni mwa wapinzani wa kisiasa na watu wa makabila fulani.
Mnamo mwaka wa 2005 Ubelgiji ilitoa waranti wa kuwezesha kukamatwa kwa Habre baada mwananchi wa Ubelgiji mwenye nasaba ya Chad kuwasilisha malalamiko dhidi ya Habre mnamo mwaka 2000.
Mwandishi: Stumai george/AFP/DPA
Mhariri:Mtullya Abdu