Mashirika ya ndege Afrika yasitisha safari za China
31 Januari 2020Barani Afrika shirika la ndege la Kenya Airways na lile la Rwandan Air yamefuta safari zake zote za kwenda na kutoka China kwa muda usiojulikana. Mpaka sasa zaidi ya watu 200 wameshakufa huko China.
Kufikia sasa kirusi cha Corona kimeshaingia kwenye nchi 18 duniani ambapo Marekani imethibitisha visa 6 vya watu walioambukizwa kufikia sasa wakati Ujerumani nako imethibitishwa kwamba watu watano wameambukizwa.
Nchi mbali mbali zimeongeza juhudi za kukabiliana na kirusi hicho ikiwemo za barani Afrika ambako mamlaka za Kenya zimetuma nchini Afrika Kusini sampuli ya damu ya mtu anayeshukiwa kuambukizwa kirusi hicho kipya ili ifanyiwe uchunguzi zaidi.
Mgonjwa huyo amewekwa katika wodi maalum katika hospitali ya Nairobi baada ya kuchukuliwa alipowasili siku ya Jumanne kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Guangzhou, Kusini mwa China. Shirika hilo la ndege la Kenya limetangaza kwamba linasimamisha safari zake zote za ndege za kutoka na kuingia kutoka Guangzhou China kuanzia leo ijumaa kwa kipindi kisichojulikana.
Shirika la ndege la RwandaAir pia limefuta safari zake za kuelekea kwenye mji huo wa kibiashara wa China likisema kwamba uamuzi huo utatathminiwa upya mwezi Februari. Alhamis shirika kubwa kabisa la ndege barani Afrika,Ethiopia Airline lilikanusha ripoti kwamba litasimamisha safari zake za ndege za kuelekea China baada ya kituo chake cha mawasiliana ya simu kuliambia shirika la habari la Reuters kwamba safari zake za ndege zimefutwa.
Shirika la afya duniani WHO jana lilitangaza kirusi cha Corona kuwa ni dharura ya kiafya duniani wakati kirusi hicho kikiendelea kusambaa kwa kasi. Kutoka Wuhan ambako ni kitovu cha ugonjwa wa homa ya Corona, msemaji wa Hospitali kuu ya mji Wang Jiliang anasema wanajizatiti kupambana na ugonjwa huo.
Taharuki inaongezeka miongoni mwa idadi inayokadiriwa kuwa maelfu ya wanafunzi wa kiafrika walioko mji huo wa Wuhan. Chama cha wanafunzi kutoka Ethiopia leo kimetowa taarifa inayosema kwamba wanafunzi wanadai kurudishwa nchini mwao haraka iwezekanavyo. Kuna takriban wanafunzi 300 kutoka Ethiopia katika mji huo wa Wuhan.Ujerumani imepeleka ndege kuwahamisha raia wake 100 walioko kwenye mji huo wa Wuhan.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Iddi Ssessanga