1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika: Waondoeni wahouthi kwenye orodha ya magaidi

25 Januari 2021

Mashirika 22 ya msaada wa kiutu yanayofanya kazi nchini Yemen yamemtolea wito rais wa Marekani Joe Biden kuwaondoa waasi wa Houthi kutoka orodha ya makundi ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/3oMMt
Jemen 2015 | Houthi-Rebellen bei Bab al-Mandab
Waasi wa Houthi wanadhibiti mji mkuu wa Yemen, Sanaa, tangu mwaka 2014Picha: picture-alliance/AP Photo/W. Qubady

Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa siku ya Jumapili,  makundi hayo yamesema uamuzi wa kuwaorodhesha waasi wa Houthi kuwa magaidi unatishia pamoja na mambo mengine kuvuruga usambazaji wa msaada wa kiutu nchini Yemen katika wakati baa la njaa linaandama nchi hiyo.

Makundi hayo ya msaada ikiwemo shirika la Oxfam na Save the Children yametahadharisha kwamba waasi wa Houthi wanaweza kusababisha kuchelewa kufikishwa huduma muhimu za kiutu au kuzuia kabisa msaada huo kuyafikia maeneo mengi ya Yemen.

Uamuzi wa kuwataja waasi Houthi kuwa kundi la kigaidi ulipitishwa na utawala ulioondoka madarakani nchini Marekani wa Donald Trump na ulianza kufanya kazi siku moja kabla rais Biden hajaapishwa kuchukua hatamu za uongozi.

Makundi hayo kwa pamoja yanamtaka Biden kuondoa amri hiyo yakisema, Yemen taifa lililo vitani kwa zaidi ya miaka sita litashuhudia hali mbaya zaidi iwapo uamuzi huo wa Marekani hautabatilishwa.

Maisha ya watu yatakuwa hatarini nchini Yemen 

Jemen Kinder im Flüchtlingslager in der Provinz Hajjah
Utapiamlo na ukosefu mkubwa wa chakula ni miongoni mwa madhila yanayoikumba Yemen.Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Al Wafi

"Mparaganyiko wowote kwenye shughuli za kiutu na uingizaji chakula, nishati, dawa na bidhaa nyingine zitayaweka rehani maisha ya mamilioni ya watu" imesema sehemu ya taarifa ya mashirika hayo 22.

Mashirika hayo yameonya kuwa hasira za waasi wa Houthi kwa uamuzi huo wa Marekani zitazidisha makali ya mzozo wa kibinaadamu na kuongeza kishindo kwa jamii ya wayemen ambao tayari vita, janga la virusi vya corona na baa la njaa vimesababisha madhila yasiyoelezeka.

Kadhilika uamuzi huo unatishia kuvuruga juhudi za Umoja wa Mataifa za kutafuta amani ya kudumu nchini Yemen.

Tangu mapema mwezi huu Umoja wa Mataifa ulikwishatoa wito kwa Marekani kubadili hatua hiyo ya utawala wa Trump.

Miito katikati ya juhudi ya kufikia amani ya kudumu Yemen 

Miito hiyo imetolewa katika wakati pande zinazohasimiana nchini Yemen, zimeanza tena  mazungumzo yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya kubadilishana wafungwa.

Jemen Konfliktparteien vereinbaren Gefangenenaustausch
Pande hasimu zikishiriki mazungumzo ya kubadilishana wafungwa Picha: Fabrice Coffrini/AFP

Miezi mitatu tangu kufanyika ubadilishanaji wa kwanza na mkubwa zaidi wa wafungwa 1,000 baina ya serikali na waasi wa Houthi, mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalianza tena jana Jumapili kwenye mji mkuu wa Jordan, Amman.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen martin Griffiths amewahimiza washiriki wa mkutano huo kuwapa kipaumbele wafungwa ambao ni wagonjwa, walio na majeraha, vikongwe, watoto na wanawake kwa kuachiliwa mara moja bila msharti.

Mzozo wa Yemen ulioanza tangu vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasia kwenye madola ya kiarabu hadi sasa umesababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni wengi kuyakimbia makaazi yao.