1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika: Adhabu ya kifo Tanzania ifutwe

10 Oktoba 2024

Mashirika ya kutetea haki za binadamu Tanzania yametoa wito kwa mamlaka kutupa jicho na kufuta adhabu ya kifo ambayo haijatekelezwa kwa zaidi ya miaka 30 huku wafungwa wake wakiendelea kusubiri adhabu hiyo.

https://p.dw.com/p/4ldq7
Chumba cha kutekeleza hukumu ya kifo
Chumba cha kutekeleza hukumu ya kifo Picha: Nate Jenkins/AP/picture alliance

Mashirika hayo ambayo Alhamis  yalikusanyika pamoja kama sehemu ya kuadhimisha siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani yanasema adhabu hiyo siyo tu kwamba inatweza utu lakini pia inakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.

Licha ya Tanzania kuwa na makosa ya aina tatu yanayotoa adhabu ya kifo, ambayo kuua kwa kukusudia, uhaini pamoja na yale ya kijeshi, hata hivyo kwa zaidi ya miaka 30 sasa hakuna mfungwa yoyote aliyenyongwa hali ambayo inawapa msukumo watetezi wa haki za binaadamu kuona kutokokuwa na haja ya kuendelea na adhabu hiyo.

Adhabu ya kifo itupiliwe mbali

Wanaharakati wanataka serikali kuchukua mkondo mwingine na kuleta adhabu mbadala ambayo wanasema itazingatia utu wa binadamu na kuheshimu mikataba ya kimataifa.

Wakili Elizibeth Majagi wa shirika la msaada kwa wanawake na haki jinai ameishauri serikali kuitupilia mbali adhabu hiyo na kwamba inaweza kufanya hivyo kwa kukaribisha adhabu mbadala ambayo itazingatia haki za binadamu na utu wake.

Wanaharakati Marekani wkaipinga hukumu ya kifo
Wanaharakati Marekani wakipinga hukumu ya kifoPicha: Allison Bailey/NurPhoto/picture alliance

Wanaharakati hao wanasema Tanzania inaweza kutekeleza hatua za kuiondoa adhabu hiyo ikiwemo pia kwa kufuata mapendekezo ya ripoti ya tume ya haki jinai ambayo pamoja na mambo mengine iliweka uzito kuhusu eneo hilo la adhabu ya kifo.

Wafungwa waandamwa na hali ngumu

Mkurugenzi mkuu wa kituo cha sheria na haki za binadamu, Dr Anna Henga anakwenda mbali zaidi kuhusu hatua zinazoweza kufanikisha uuondoshwaji wa adhabu hiyo ikiwamo pamoja kufuata maazimio ya kimataifa.

Rose Male ambaye kwa wakati fulani alitiwa hatiani na kuhukumiwa ya adhabu ya kunyongwa hadi kufa kabla ya kukata rufani na kushinda amekuwa na ushuhuda kuhusu hali ngumu inayowaandama wafungwa wengi walioko gerezani ikiwamo wale wanaosubiri kunyongwa.

Kwa muda mrefu sasa Umoja wa Mataifa umekuwa ukizihimiza nchi wanachama wake zinazoendelea kutekeleza adhabu ya kifo kuchukua mkondo mpya wa kuondoa adhabu hiyo ikisisitiza kuwa utekelezaji wake unakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.