Mashindano ya Olimpiki ya Rio yamalizika rasmi
22 Agosti 2016Ni kwaheri ya kuonana kutoka Rio de Janeiro , wakati mashindano makubwa duniani ya olimpiki yalikamilika na kufikia tamati kwa mwaka huu, wakati kijiti cha olimpiki kikichukiliwa na mji wa Tokyo nchini Japan ambao utatayarisha mashindano hayo mwaka 2020.
Baada ya wiki mbili za michezo mbali mbali nje na ndani ya viwanja , pamoja na mambo mengine yaliyofurahisha na kuchafua heba ya michezo hiyo , rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach aliisifu michezo hiyo iliyofanyika katika mji huo wa Brazil.
Michezo hii ya olimpiki imeacha urithi adimu kwa vizazi vijavyo. Historia itazungumzia kuhusu Rio de Janeiro kabla na Rio iliyobora zaidi baada ya michezo hii ya Olimpiki.
"Sasa natangaza rasmi michezo hii ya 31 ya Olimpiki imefungwa."
Saa chache kabla ya kufungwa mashindano hayo, kikosi cha timu ya mpira wa kikapu cha Marekani kilishinda medali ya dhahabu ya mwisho katika mashindano hayo , kikiimarisha nafasi ya nchi hiyo katika orodha ya nchi zilizovuna medali medali nyingi katika michezo hiyo.
Katika sherehe za kufunga michezo hiyo , maelfu ya mashabiki na wachezaji walivalia wazi maarufu la America ya kusini la Poncho katika usiku ambao ulikuwa na mvua na upepo wakishuhudia tamasha la kupendeza la utamaduni wa Brazil na musiki pamoja na fashifashi zikilipuliwa angani katika uwanja wa Maracana.
Wakitabasamu na wakipunga mikono wanamichezo walicheza ndani ya uwanja wa Maracana wakipiga picha za ukumbusho wakati michezo hiyo ya majira ya joto mjini Rio ikifikia mwisho na kujitayarisha kwa michezo ya mjini Tokyo mwaka 2020.
Japan kushika kijiti cha Olimpiki
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema hapo kabla wakati alipokutana na wanamichezo wa Japan walioshinda medali kwamba serikali ya Japan itafanyakazi kwa bidii kuhakikisha michezo hiyo inakuwa ya mafanikio makubwa.
Kitisho cha usalama na matatizo ya usafiri ni hali iliyokuwapo katika michezo hii ya kwanza kufanyika katika ardhi ya America kusini , iliyofanyika katika wakati wa matatizo ya kisiasa na kiuchumi nchini Brazil.
Katika siku ya mwisho ya mashindano hayo , Eliud Kipchoge wa Kenya , mwenye umri wa miaka 31 aling'ara akifikisha ushindi wake wa saba katika mbio ndefu za marathon akimaliza kwa saa 2 dakika 8 na sekunde 44, akishinda kwa zaidi ya dakika moja. Bismark Mutahi alishuhudia mbio hizo.
Medali ya mwisho ya dhahabu
Kwa ushindi wa timu ya mpira wa kikapu ya Marekani , nchi hiyo ilifikisha jumla ya medali 46 za dhahabu na kufikia kiwango ilichopata katika michezo ya London miaka minne iliyopita na kuongoza orodha ya nchi zilizopata medali nyingi, na Uingereza ikawa ya pili kwa kujikingia medali 27 na China ya tatu ikijikingia medali 26 za dhahabu.
China imepelela mjini Rio kikosi cha vijana chipukizi wenye umri wa wastani wa miaka 24 , licha ya kwamba mashindano haya yamekuwa mabaya zaidi kwa nchi hiyo ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo ilishika nafasi ya pili mjini London.
Brazil iliripuka kwa furaha pale timu yao ya soka iliponyakua medali ya dhahabu, medali ambayo imeeenziwa sana na mashabiki wa nchi hiyo kiasi cha kusahau matatizo ya nchi hiyo kwa muda.
Lakini mara nyingi kandanda katika olimpiki ni mchezo ambao nchi za mataifa ya Ulaya hazitilii umuhimu wa juu kama zilivyo nchi za America kusini na Afrika.Lakini baada ya Brazil kunyakua medali ya dhahabu kwa mara ya kwanza katika historia katika michezo hii, hata Ujerumani iliyoridhika na medali ya fedha ilitafakari ushiriki wake. "Tunapaswa kuchukulia kwa dhati kandanda katika Olimpiki hapo baadaye," amesema kocha Horst Hrubesch.
Kwingineko katika soka;
Ligi za barani Ulaya zinaendelea ambapo katika La Liga Gareth Bale alipachika mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0 wa Real Madrid dhidi ya Real Sociedad jana Jumapili , akirudia kile alichokifanya katika michezo ya Euro 2016 nchini Ufarnsa kwa timu yake ya taifa ya Wales.
Mahasimu wao Atletico Madrid hata hivyo waliambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Alaves waliopanda daraja msimu huu. Hapo kabla Sporting Gijon waliishinda Atheletic Bilbao kwa mabao 2-1 na mabingwa watetezi Barcelona waliwararua bila huruma Real Betis kwa mabao 6-2.
Nchini Uingereza mbinyo mkubwa uko kwa kocha wa Sunderland David Moyes na Arsene Wenger wa Arsenal , timu ambazo hadi sasa baada ya michezo miwili hazijapata ushindi.
Meneja wa Sunderland david Moyes amewaonya mashabiki wa timu hiyo kujitayarisha kwa mapambano ya kushuka daraja kwa msimu wa tano mfululizo baada ya timu yake kushindwa kwa mara ya pili mfululizo katika Premier League, mara hii dhidi ya Middlesbrough.
Nahodha wa zamani wa Arsenal Patrick Vieira anamuunga mkono meneja Arsene Wenger katika kubana matumizi kununua wachezaji lakini alisema wachezaji zaidi watahitajika kufuatia kikosi hicho cha kaskazini mwa jiji la London kinavyofanya katika michezo ya mwanzo ya Premier League.
Arsenal iliridhika na sare ya bila kufungana na mabingwa wa ligi hiyo Leicester City siku ya Jumamosi baada ya kushindwa katika mchezo wake wa mwanzo dhidi ya Liverpool.
Katika Champions League,
Manchester City na Borussia Moenchengladbach ziko katika nafasi nzuri ya kufikia awamu ya makundi ya Champions League. Monaco, Legia warsaw, Celtic, Ludogorets na Copenhagen pia zina ushindi kuingia katika michezo ya mkondo wa pili wa michuano ya mchujo kesho Jumanne na Jumatano.
Manchester City na Moenchengladbach zinaingia katika mchezo utakaopigwa nyumbani kwao kwa ushindi mkubwa , wakati Monaco na Legia warsaw ni timu nyingine mbili zikiwa na ushindi katika mchezo wa mkondo wa kwanza.
Sergio Aguero alipachika mabao matatu wakati Manchester City ilipoishindilia Steua nyumbani kwao kwa mabao 5-0. Kocha wa Manchester City Pep Guardiola atawapumzisha baadhi ya wachezaji lakini hakuna hakika kwamba mlinda mlango Joe Hart atarejea langoni. Hart anafikiriwa huenda akahamia Everton wakati City wanatarajiwa kukamilisha uhamisho wa mlinda mlango wa Barcelona Claudio Bravo wiki hii.
Katika bara la Afrika
Wydad Casablanca ya Morocco inahitaji pointi moja tu itakapocheza na Zesco United ya Zambia siku ya Jumatano kushika nafasi ya kwanza katika kundi A na kuweza kupambana na zamalek ya Misri katika mpambano wa nusu fainali.
Lakini iwapo mabingwa hao wa Afrika mwaka 1992 watashindwa katika uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola na Zesco United , wataporomoka hadi nafasi ya pili na kukumbana na washindi wa kundi B Mamelodi Sondowns ya Afrika kusini badala yake.
Klabu ya Algeria ya Mouloudia Bejaia inaweza kufikia nusu fainali hizo kesho baada ya kupachika bao lao la pili katika michezo sita ya kundi A iliyocheza.
ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Medeama ya Ghana katika duru ya mwisho unawachukua Waalgeria hao hadi katika kuwa sare kwa mabao na pointi licha ya ukame huo wa mabao na timu hiyo ya Ghana.
TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo , ina wachezaji kutoka Congo, Ghana, Cote d'Ivoire , Mali, tanzania na zambia , inahitaji pointi moja tu nayo wakati itakapopambana na Dar Young Africans , Yanga ya dar es Salaam na kuwa na uhakika wa kuwa juu ya kundi hilo.
mabingwa wa zamani FUS Rabat ya Morocco na mabingwa watetezi Etoile Sahel ya Tunisia zimefuzu kuingia katika nusu fainali kutoka kundi B.
Na kwa taarifa hiyo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo jioni ya leo. Jina langu ni Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Mohammed Khelef