Mashindano ya olimpiki kuanza Ijumaa
1 Agosti 2016Zimebakia siku nne hadi kuanza rasmi michezo ya 31 ya Olimpiki mjini Rio. Mahakama ya kimataifa ya michezo inachukua hatua za haraka kuamua rufaa zilizopelekwa katika mahakama hiyo na wanariadha wa Urusi kupinga marufuku ya kushiriki michezo ya Rio ambapo sherehe za ufunguzi zinatarajiwa kufanyika mnamo siku nne zijazo.
Hatua ya kuzuiwa kwa njia mpya ya treni kwa ajili ya eneo la michezo hiyo ya Olimpiki ni moja katika ya changamoto zilizowakabili watayarishaji wa michezo hiyo pamoja na kuweza kuweka viwanja pamoja na vifaa kuwa tayari kwa ajili ya michezo hiyo.
Wanamichezo kadhaa wa Urusi wamepeleka katika mahakama hiyo rufaa ya kutaka kuruhusiwa kushiriki katika michezo hiyo baada ya shirika linalopambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli, doping kugundua kuwa kulikuwa na utaratibu wa kitaifa kuwapa wanamichezo wa nchi hiyo dawa hizo.
Pamoja na hayo hewa katika jiji la Rio de Janeiro inasemekana kuwa ni chafu na yenye madhara kuliko ilivyoelezwa na maafisa na walivyoahidi.
Lakini kwa upande mwingine kuna habari za kutia moyo , baada ya maafisa wa afya wa Brazil kusema jana kwamba kitisho cha ugonjwa hatari wa Zika ni cha chini katika michezo hiyo ya olimpiki.
Waziri wa afya wa Brazil Daniel Soranz , amesema virusi vya zika haviwezi kuzuwia wasafiri kwenda katika michezo hiyo, wakati maambukizi ya virusi hivyo yameshuka kwa kiasi kikubwa katika miezi ya hivi karibuni.
Timu zinajiandaa kwa msimu mpya
Vilabu mbali mbali nchini Ujerumani na kwingineko katika bara la Ulaya vinajitayarisha na msimu ujao ambao utaanza rasmi mwezi huu. Nchini Ujerumani mabingwa Bayern Munich wako nchini Marekani wakijitayarisha kwa msimu ujao, licha ya kuwakosa hadi sasa majogoo wao wengi ambao wamehusika katika michuano ya kombe la Ulaya Euro 2016 iliyomalizika nchini Ufaransa mwezi uliopita.
Makamu bingwa Borussia Dortmund imekamilisha usajili wa wachezaji wanane ambao wataimarisha kikosi hicho kinachoongozwa na kocha Thomas Tuchel. Wachezaji waliojiunga leo ni pamoja na Mario Goetze aliyetokea Bayern Munich na kurejea nyumbani , Andre Schurrle kutoka Wolfsburg,na Rafael Guerreiro bingwa wa Ulaya akiwa na Ureno.
Schalke 04 imeimarisha kikosi chake mwishoni mwa juma hili kwa kumnyakua mlinzi wa Sevilla ya Uhispania Coke.
Sane aelekea Man City
Wakati huo huo Leroy Sane mshambuliaji wa Schalke 04 ameelekea Uingereza hii leo akitarajiwa kuhamia nchini humo katika klabu ya Manchester City, imesema klabu hiyo ya Bundesliga leo.
Sane mwenye umri wa miaka 20 , ambaye hakusafiri na timu hiyo ya Bundesliga kwenda katika kambi ya mazowezi nchini Austria , alipachika mabao manane pamoja na kutayarisha mengine sita kwa Schalke msimu uliopita wakati timu hiyo ikimaliza katika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi.
Kijana huyo aliomba kuondoka Schalke , alithibitisha mkurugenzi wa klabu hiyo mwezi uliopita, na vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kwamba makubaliano yanaweza kuipatia Schalke kitita cha pauni milioni 30.
Nchini Uingereza Manchester United imejiimarisha chini ya kocha mpya Jose Mourinho na inatarajiwa kutoa changamoto kali kuelekea ubingwa wa Premier League, amesema nahodha wa timu hiyo Wayne Rooney.
Nahisi wachezaji wanajisikia kuwa hii ni Manchester mpya . Sio tu kuhusu wachezaji wapya , tuna Anthony Martial na Marcus Rashford kutoka msimu uliopita ambao walionyesha uwezo mkubwa, amesema Roooney katika mahojiano na gazeti la Daily Mail.
Diego Costa huenda akarejea alikotoka
Kocha wa Chelsea Antonio Conte hana hakika juu ya majaliwa ya mshambuliaji Diego Costa , wakati vyombo vya habari nchini Uhispania vikiripoti kuwa mshambuliaji huyo huenda akarejea katika klabu yake ya zamani ya Atletico Madrid.
Arsenal London imemaliza ziara yake nchini Marekani kwa ushindi wake wa pili dhidi ya Chivas Guadalajara ya Mexico kwa mabao 3-1.
Wakati huo huo hapa nchini Ujerumani kumekuwa na majadala kuhusiana na nani atakuwa nahodha wa timu hiyo mabingwa wa dunia baada ya nahodha Bastian Schweinsteiger kuamua kuweka madaluga darini kwa timu ya taifa.
Baadhi ya wadadisi wa masuala ya soka wanafikiria kwamba wakati umefika sasa kuwa na nahodha ambaye anatoka katika jamii mchanganyiko. Mchezaji ambaye ni Mjerumani , mazaliwa wa Ujerumani, lakini ama kachanganya damu ama anaasili ya nje ya nchi hii. Kuna orodha ya wachezaji wa muda mrefu katika timu hiyo kama Sami Khedira, Mesut Ozil, na mlinzi shupavu Jerome Boateng ambaye mzazi wake wa kiume anaasili ya Ghana.
Simba kampuni
Nchini Tanzania moja kati ya timu kigogo katika ligi ya nchi hiyo Simba Sports Club inajiandaa kuingia katika mfumo mpya wa uendeshaji kandanda katika klabu hiyo kwa kuamua kuwa kampuni itakayoiendesha kabla ya mpira.
Klabu hiyo jana ilikuwa na mkutano wake wa kila mwaka ambapo moja ya mada zilizojadiliwa ni mfumo wa kampuni itakayouza hisa. Mmoja kati ya wadau wakubwa wa klabu hiyo tajiri Mohammed Deuji ameahidi kuipatia Simba kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni 20 kuendeleza klabu hiyo katika nyanja mbali mbali na kuanzisha mfumo huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Gakuba Daniel