Mashariki ya Kati Magazetini
6 Januari 2014Tuanzie lakini Mashariki ya kati ambako gazeti la mjini Berlin "Berliner Zeitung" linazungumzia matarajio ya kuona juhudi za waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry zikileta tija.Gazeti linaendelea kuandika:"Kila kitu kitategemea kama John Kerry katika ziara zake nchini Jordan na Saud Arabia,atafanikiwa kupata uungaji mkono wa wafalme wa nchi hizo kwa mpango wake wa amani.Hiyo itakuwa karata yeye nguvu kuweza kuwatanabahisha Benjamin Netanyahu na Mahmoud Abbas.Bado ufumbuzi wa madola mawili upo na unawezekana.Pindi John Kerry akishindwa katika juhudi zake,basi miaka itapita,hakuna yeyote mwengine atakaejibwaga katika mzozo huo unaotishia wakati wowote ule kuripuka.Na ndio maana,kilichosalia ni kimoja tu ,nacho ni kumuombea ufanisi John Kerry!"
Mzozo wa Iraq na Syria nao pia umewashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani.Gazeti la "Nürnberger Zeitung" linaandika:"Mashaka yanayozidi kuongezeka nchini Iraq na Syria yanabainisha kwa mara nyengine tena hali tete iliyoko kati ya waumini wa madhehebu ya shiya na sunni katika eneo jumla la Mashariki ya kati.Haitakuwa kutia chunvi watu wakizungumzia hatari ya kuripuka vita vya kimadhehebu."
Tunisia Yasifiwa
Kinyume na kitisho kinachotanda Iraq na Syria,nchini Tunisia hali imeanza kupambazuka.Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linaandika:"Uamuzi wa bunge la Tunisia wa kutoitumia Qoraan kuwa mwongozo wa sheria nchini humo unastahiki sifa.Vifungu viwili vya mwanzo vinazungumzia wazi kabisa kuhusu "jamhuri ya kiraia."Hakuna njia kwa hivyo ya kubadilishwa siku za mbele na kuwa nchi ya utawala unaofuata sharia ya dini ya kiislam.Hali hiyo inakumbusha kile kifungu cha sheria msingi ya Ujerumani kinachozuwia uwezekano wa Ujerumani kutumbukia siku moja katika zile enzi za kale za kiimla.Na hali hiyo inatofautiana pia na ile inayoshughudiwa hasa nchini Syria na Iraq.Huko makundi yanayoelemea upande wa Al Qaida yanaonyesha kusonga mbele na kutangaza sheria ya kiislam katika kila eneo linaloangukia mikononi mwao."
Wladimir Putin ajigeuza Kinyonga
Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Urusi.Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linamulika michezo ya Olympik ya msimu wa baridi huko Sotchi na kuandika:"Wladimir Putin anajigeuza mwanademokrasia halisi.Kiongozi wa ikulu ya Urusi-Kremlin anataka kuitakasa sifa yake mbaya ya muimla,ili kuuokoa mradi wake wa mabilioni ya fedha-michezo ya Olympik ya msimu wa baridi huko Sotchi.Hakuchelea kuregeza kamba na kufika hadi ya kuruhusu watu waandamane.Lakini tusidanganyike:Haimaanishi kwamba Putin anaruhusu uhuru wa watu kutoa maoni yao.Serikali yake ndio inayoamua kuhusu mahala,wakati na nini cha kulalamikiwa."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman