1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaitikisa tena Nairobi

15 Januari 2019

Washambuliaji wanaoaminika kuwa magaidi wameshambulia katika hoteli moja iliyoko kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

https://p.dw.com/p/3BbE1
Kenia Nairobi Explosion und Schüsse in Hotel und Bürogebäude
Picha: Reuters/T. Mukoya

Mji huo umetikiswa na miripuko ya mabomu na ufyatulianaji risasi kati ya vikosi vya usalama na washambuliaji, katika shambulizi ambalo polisi na walioshuhudia wamelitaja kuwa la kigaidi. Maafisa wa usalama wako kwenye eneo la tukio wakijaribu kuwaokoa watu na polisi wamethibitisha kutokea kwa shambulio hilo kwenye eneo la Riverside.

Msemaji wa Polisi, Charles Owino amesema maafisa zaidi wa polisi ikiwa ni pamoja na vikosi vya kupambana na ugaidi wamepelekwa katika eneo la tukio. Magari ya kubeba wagonjwa na askari wa zimamoto wameshapelekwa katika eneo hilo. Aidha, magari kadhaa yamewaka moto, likiwemo lile lililotumiwa na washambuliaji.

Taarifa zinaeleza kuwa watu kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo ambalo limetokea kwenye jengo kubwa lenye hoteli kubwa inayoitwa DusitD2 pamoja na maduka mengine na benki.

Kenia Nairobi Explosion und Schüsse in Hotel und Bürogebäude
Askari wakionekana katika eneo la shambuliziPicha: Reuters/T. Mukoya

Hata hivyo, mtu mmoja aliyeshuhudia Robert Murire amesema ameona kiasi ya miili miwili katika eneo la tukio, sambamba na washambuliaji waliokuwa wamevalia nguo za rangi ya kijani na wakiwa wamejifunga mikanda ya risasi.

Mkuu wa Polisi nchini Kenya, Joseph Boinnet amesema katika taarifa yake wanafahamu kwamba wahalifu hao wenye silaha bado wako ndani ya hoteli hiyo. Amebainisha kuwa vikosi maalum kwa sasa vinajaribu kuwaondoa.

Al-Shabaab yakiri kuhusika

Kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab limedai kuhusika na shambulizi hilo na limesema wapiganaji wake bado wako ndani ya jengo hilo. Kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, limetangaza taarifa hiyo kupitia redio yake ya Andalus.

Shambulizi hili linalikumbusha lile la mwaka 2013 katika jengo kubwa la maduka la Westgate, ambapo wanangambo hao wenye itikadi kali waliwaua kiasi ya watu 67.

Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umetangaza tahadhari ya kiusalama kwa raia wake na umewashauri kukaa mbali na eneo hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga