1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Urusi yawaacha watu milioni bila umeme

28 Novemba 2024

Urusi imefanya mashambulizi ya pili kwa ukubwa mwezi huu katika miundo mbinu ya nishati ya Ukraine Alhamis na kusababisha ukosefu wa umeme kwa watu milioni moja magharibi, kusini na eneo la kati la nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4nX0b
Afisa wa zima moto akiwa kazini baada ya shambulizi la Urusi Ukraine
Afisa wa zima moto akiwa kazini baada ya shambulizi la Urusi UkrainePicha: UKRAINIAN EMERGENCY SERVICE/Handout/AFP

Haya yanafanyika wakati ambapo Ukraine imeituhumu Urusi kwa kufanya uhalifu wa kivita katika eneo la kusini la Zaporizhzhiya.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema jeshi lake limerusha zaidi ya makombora 90 na ndege 100 zisizokuwa na rubani, akidai shabaha 17 zililengwa.

Baada ya shambulizi hilo, zaidi ya watu milioni moja wameachwa bila umeme nchini Ukraine kuliko na kibaridi kikali.

Kombora la Oreshnik lageuza chochote kuwa mavumbi

Rais huyo wa Urusi ameongeza jeshi lake limefanya mashambulizi hayo kama jawabu la Ukraine kufanya mashambulizi katika mipaka ya Urusi kwa kutumia makombora ya masafa ya kati ya Marekani.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Gavriil Grigorov/POOL/AFP

"Kama ambavyo imesemwa awali, tutajibu mashambulizi yanayoendelea kufanywa nchini Urusi kwa makombora ya nchi za Magharibi. Upo uwezekano kwamba tutaendelea kuyafanyia majaribio makombora ya Oreshnik katika mazingira ya kijeshi kama ilivyofanyika Novemba 21. Kwa sasa wizara ya ulinzi na mkuu wa utumishi katika Jeshi la Urusi wanatafuta maeneo ya kulenga ndani ya Ukraine. Maeneo haya yanaweza kuwa vifaa vya kijeshi, kampuni za ulinzi au vituo vya kufanyia maamuzi vya Kyiv," alisema Putin.

Putin alidai kombora jipya la Oreshnik ambalo wataendelea kulifanyia majaribio,linaweza kusambaratisha kitu chochote kile na kukifanya kiwe mavumbi, huku akisema Urusi inafahamu idadi kamili ya makombora ya masafa marefu iliyopewa Ukraine na sehemu yalipo.

Kwa upande wake Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameituhumu Urusi kwa kuvitanua vita hivyo. Wizara ya ndani ya Ukraine imesema uharibifu wa miundo mbinu imefanyika katika maeneo tisa kote nchini humo.

Maafisa wa Ukraine walisema makombora na droni zote zilizokuwa zimeelekezwa mji wa Kyiv zilidunguliwa. Mji huo mkuu wa Ukraine umezungukwa na mifumo thabiti ya ulinzi wa angani.

Ukraine kuandaa mkutano wa kilele wa amani kusitisha uvamizi wa Urusi

Hayo yakiarifiwa Ukraine inasema jeshi la Urusi limefanya uhalifu wa kivita katika eneo la Zaporizhzhya ambako wanajeshi watano kati ya sita wa Ukraine, walipigwa risasi na kuuwawa baada ya kukamatwa karibu na kijiji cha Novodaryivka.

Shambulizi la Urusi lililoharibu kampuni ya umeme Kyiv
Shambulizi la Urusi lililoharibu kampuni ya umeme KyivPicha: Vyacheslav Madiyevskyy/Ukrinform/ABACA/IMAGO

Kulingana na afisi ya mwendesha mashtaka mjini Kyiv, tukio hilo lilifanyika siku ya Jumamosi na kwamba kwa sasa, uchunguzi wa uhalifu wa kivita na mauaji unaendelea.

Wakati huo huo, mkuu wa utumishi wa rais nchini Ukraine, Andriy Yermak, amesema Alhamis kuwa nchi hiyo iko tayari kuandaa mkutano wa kilele wa dunia hivi karibuni unaolenga kuumaliza uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Ukraine ilifanya mkutano wake wa kwanza wa kilele wa amani nchini Uswisi mnamo mwezi Juni, ambapo ilizileta pamoja zaidi ya nchi 90 kurasimu azimio lililokuwa na mapendekezo ya masharti ya Ukraine, kwa ajili ya kusitisha vita hivyo.

Urusi haikualikwa kwenye mkutano huo wa kilele na kudai kwamba yaliyojadiliwa hayakuwa na maana bila uwepo wake.

China pia haikuhudhuria mkutano huo wa kilele huku nchi nyengine zenye nguvu na ambazo si za Magharibi zikichelea kutia saini yaliyokubaliwa kwenye mkutano huo wa kilele.

Vyanzo: DPAE/Reuters/AFP